Twiga Kings
Michezo Bongo

Twiga Kings Yapewa Masharti Magumu Safari ya Afrika Kusini

Vardo October 21, 2026 7:17 pm

OFISA wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Charles Maguzu, ameitaka timu ya taifa ya rugby ya wanaume, Twiga Kings, kwenda Afrika Kusini kupambana kwa nguvu zote katika mashindano ya Obaro 7s na kurejea nchini ikiwa na medali.

Twiga Kings inatarajiwa kushiriki mashindano hayo yatakayofanyika jijini Pretoria, Oktoba 24 na 25 mwaka huu, huku kikosi hicho kikitarajiwa kuondoka nchini Oktoba 22 kuanza safari ya kuwakilisha Tanzania katika jukwaa hilo la kimataifa.

Maguzu amesema ushiriki wa timu hiyo haupaswi kuwa wa kutimiza ratiba pekee, bali ni fursa ya kuonyesha uwezo wa raga ya Tanzania, kupambana na wapinzani wenye ushindani mkubwa na kuitangaza nchi kupitia mafanikio ya michezo.

Akizungumzia umuhimu wa mashindano hayo, Maguzu amesisitiza kuwa ushiriki wa kimataifa ni sehemu muhimu ya kukuza uwezo wa wanamichezo, kwa kuwa unawapa nafasi ya kupima viwango vyao, kupata uzoefu na kujifunza mbinu mpya za ushindani.

“Kuendeleza michezo nchini kunahitaji zaidi ya kuandaa wanamichezo kwa ajili ya mashindano. Tunahitaji kuwekeza katika vipaji, kuimarisha taasisi za michezo, kuwaongezea uwezo wanamichezo na kuweka ushirikiano utakaowapa nafasi za kuendelea mbele,” amesema Maguzu

SPORTPESA, TRU WAPONGEZWA

Katika hatua nyingine, Maguzu amepongeza ushirikiano kati ya Kampuni ya SportPesa na Chama cha Rugby Tanzania (TRU), akieleza kuwa mchango wa wadau ni muhimu katika kukuza na kuimarisha mchezo huo nchini.

Amesema ushirikiano huo unatoa fursa kwa timu za Tanzania kushiriki mashindano ya ndani na nje ya nchi, jambo linalosaidia kukuza vipaji, kuongeza uzoefu wa wachezaji na kuimarisha ushindani.

Kwa mujibu wa Maguzu, timu zinapopata nafasi ya kushiriki mashindano ya kimataifa, zinajifunza kutokana na ushindani wa kiwango cha juu na kupata uzoefu unaoweza kusaidia kuboresha viwango vyao.

“Timu zetu zinapopata nafasi ya kushindana kimataifa, zinapata uzoefu muhimu, zinakutana na ushindani wa kiwango cha juu na kusaidia kuipa michezo ya Tanzania mwonekano zaidi,” amesema.

WADAU WENGINE WAPEWA CHANGAMOTO

Maguzu amewataka wadau wengine kujitokeza kuwekeza katika michezo kwa kusaidia programu na miradi inayolenga kukuza vipaji, kuimarisha timu na kujenga msingi imara kwa kizazi kijacho cha wanamichezo.

Amesema maendeleo endelevu ya michezo yanahitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali ili kuhakikisha wanamichezo wanapata mazingira na fursa zinazowawezesha kufikia malengo yao.

Hata hivyo, ujumbe wake mkuu kwa Twiga Kings umejikita katika kuhakikisha kikosi hicho kinatumia vyema nafasi iliyopo kwa kupambana kwa uzalendo na kuwania medali.

“Tunawapongeza SportPesa na TRU kwa ushirikiano huu na tunahimiza wadau wengine kuendelea kuwekeza katika mipango itakayosaidia kuimarisha michezo nchini na kutoa fursa kwa kizazi kijacho.

Twiga Kings wasibweteke, wakapambane kwa uzalendo na kurejea nchini na medali ambazo wanaenda kuzipambania katika mashindano hayo,” amesema Maguzu.

Kwa sasa, Twiga Kings inaelekeza nguvu zake katika maandalizi ya safari ya Pretoria, ikiwa na jukumu la kupeperusha vyema bendera ya Tanzania na kupigania matokeo yatakayoongeza heshima ya rugby ya nchi katika medani ya kimataifa.

Maandalizi Tamati Mashindano ya Obaro 7s,Twiga Kings Yaivaa Afrika Kusini Sportpesa Yaendelea Kuunga Mkono Mchezo Wa Rugby, Twiga Kings Kuwakilisha Tanzania Obaro 7s