Ahmed Ally Aichana Yanga: Waache Visingizio, Wajitathmini
Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amewapiga dongo mabingwa wa jadi Yanga kwa kuwataka kuacha kutoa visingizio kila wanapopoteza michezo au kufanya mabadiliko ya benchi lao la ufundi, badala yake wajikite katika kujitathmini na kubaini mapungufu yaliyopo kwenye kikosi chao.
Kauli hiyo ya Ahmed imekuja kufuatia hatua ya uongozi wa Yanga kuvunja mikataba ya Kocha Mkuu, Manqoba Mngqithi, na Kocha wa Viungo, Chyna Mokaila, tukio ambalo limetumiwa na kiongozi huyo kuhoji mantiki ya madai ya mara kwa mara kwamba Simba hutumia “nguvu za ziada” inapokutana na wapinzani wake.
Akizungumza kuhusu mwenendo huo, Ahmed amesema kuwa kila Simba inapopata ushindi, baadhi ya viongozi na wadau wa soka kutoka kambi ya wapinzani wao wamekuwa wakitafuta sababu za pembeni badala ya kukubali uhalisia wa uwanjani.
“Baada ya kuwafunga, wanaanza kuleta sababu nyingi badala ya kuangalia ukweli wa timu zao. Wanaanza kudai tumetumia nguvu za ziada. Kama kweli sisi tumetumia nguvu za ziada, kwa nini mmefukuza Fitness Coach? Hiyo ina maana gani?” alihoji Ahmed.
Aliongeza kuwa timu zinapocheza na wapinzani wenye kasi kubwa inayodumu kuanzia dakika ya kwanza hadi ya mwisho, zinapaswa kuchunguza uwezo na maandalizi ya wachezaji wao kimwili badala ya kuelekeza lawama kwa timu pinzani.
Aidha, Ahmed alisisitiza kuwa mafanikio ya Simba yanatokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na klabu hiyo pamoja na umakini katika maandalizi, akiwakumbusha viongozi wa soka nchini kuwekeza zaidi kwenye ubora badala ya kutafuta visingizio vya mara kwa mara.
“Kama sisi tulitumia nguvu za ziada, kwa nini mmefukuza Fitness Coach? Kwetu mlileta visingizio, TRA vipi? Waliwapakia Mkongo? Wajifunze kuheshimu mpira,” alihitimisha.
Kauli hii inazidi kupasha moto ushindani wa maneno kati ya miamba hiyo miwili ya soka la Tanzania, huku ikisisitiza umuhimu wa klabu kuangalia ndani badala ya kutafuta mchawi nje pindi matokeo yanapokosekana.