Hapa Zuchu Ameshuka, Tyla Amepanda
Wakati staa wa Bongofleva, Zuchu (32), akiweka historia mpya ya kufikisha wafuatiliaji (subscribers) milioni 5 kwenye mtandao wa YouTube na kuwa msanii wa tatu wa kike Afrika kufanya hivyo, mafanikio hayo yamethibitisha pia ushindani mkali uliopo kutoka kwa mwanamuziki wa Afrika Kusini, Tyla (24).
Kwa sasa, rekodi ambazo hapo awali zilishikiliwa na Zuchu kama msanii wa kike wa pili kwa wingi wa wafuatiliaji Afrika na namba moja kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara zimechukuliwa na Tyla, ambaye anazidi kung’ara kimataifa tangu kutamba kwa kibao chake cha Water (2023).
Safari ya Zuchu na Kilele cha Afrika Mashariki
Zuchu, aliyejizolea umaarufu mkubwa kupitia ngoma yake matata Sukari (2021), ameweka alama kubwa ikiwemo kuwa mwanamuziki wa kike wa kwanza wa kike Afrika Mashariki kufikisha wafuatiliaji milioni 5 YouTube. Hata hivyo, ujio wa Tyla wenye kasi ya radi umezifanya rekodi hizo kuhamia upande wa pili. Hivi sasa, Tyla anaongoza akiwa na wafuatiliaji zaidi ya milioni 6.1, huku msanii mkongwe kutoka Misri, Sherine, akiongoza kwa milioni 6.5.
Nguvu ya Tyla na Tuzo za Grammy
Mafanikio ya Tyla hayazuiliki; yameitikisa sio tu Zuchu bali pia mastaa wakubwa wa Afrika kama vile Wizkid, Burna Boy, na Diamond Platnumz. Ushindi wake wa tuzo kubwa za kimataifa zikiwemo Grammy, MTV VMAs, na BET, umemfanya kuandika historia kama msanii wa kwanza wa Kiafrika kushinda tuzo mbili za Grammy katika kipengele cha Best African Music Performance.
Ingawa Zuchu bado anasalia kuwa kinara wa Afrika Mashariki kwa mafanikio yake ya YouTube, ushindani huu unazidi kuonyesha jinsi muziki wa Afrika unavyopiga hatua kubwa kwenye ramani ya dunia.