Steve Barker Simba SC
Simba SC

Steve Barker Anena Mazito: Lengo la Simba SC Ligi ya Mabingwa Afrika na Robo Fainali

Vardo October 27, 2026 6:49 pm

KOCHA Mkuu wa Simba SC, Steve Barker, amesema baada ya kufanikisha lengo la kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, sasa nguvu za kikosi hicho zimeelekezwa katika kufanya vizuri kwenye hatua hiyo na kutinga robo fainali ya mashindano hayo.

Barker amesema kufuzu hatua ya makundi ni sehemu ya malengo makubwa ya Simba msimu huu, akieleza kuwa baada ya kukamilisha jukumu hilo, sasa wanajipanga kwa hatua inayofuata huku wakisubiri droo ya makundi itakayowatambua wapinzani wao.

“Lengo letu kubwa lilikuwa kufika hatua ya makundi na kwa bahati nzuri tumefanikiwa. Sasa tunasubiri droo, huku lengo linalofuata likiwa kushindana vizuri kwenye hatua ya makundi na kufika hatua ya mtoano,” amesema Barker.

Akizungumzia hoja kuhusu matumizi ya nafasi za kufunga mabao, Barker amepinga madai kwamba kikosi chake bado kinahitaji kufanya maboresho makubwa katika eneo hilo, akitolea mfano wa mabao tisa ambayo Simba imefunga katika mechi mbili za hatua za awali za mashindano hayo.

“Hapana, sikubaliani nawe. Unapofunga mabao tisa katika mechi mbili, maana yake ni kwamba unatumia vizuri nafasi zako,” amesema kocha huyo.

Hata hivyo, Barker amekiri kuwa hatua ya makundi itakuwa na ushindani mkubwa zaidi kutokana na ubora wa timu zitakazoshiriki, akisisitiza umuhimu wa kikosi chake kujiandaa kwa umakini ili kukabiliana na changamoto zitakazojitokeza.

Amesema pamoja na ushindani unaotarajiwa, anaamini Simba ina uwezo wa kufanya vizuri kutokana na kiwango kinachoonyeshwa na wachezaji wake, pamoja na imani na kujiamini walikojenga kupitia matokeo mazuri katika michezo ya hivi karibuni.

Barker amesisitiza kuwa Simba inapaswa kujiandaa kwa kila mchezo kwa umakini, bila kujali itacheza nyumbani au ugenini, akieleza kuwa lengo lao ni kucheza soka chanya na kupambana kupata matokeo katika kila mchezo.

“Tunataka kushindana kwenye jukwaa la soka la Afrika, hivyo ni jukumu letu kuhakikisha tunajiandaa vizuri kwa kila mchezo wa Ligi ya Mabingwa, iwe nyumbani au ugenini. Tunapaswa kucheza kwa mtazamo chanya na kutafuta matokeo katika kila mechi,” amesema Barker.

Usajili wa Simba SC: Kauli ya Rweyemamu Yawashtua Wapinzani Dirisha Dogo Simba SC vs Fountain Gate: Simba Kutumia Babati Kuvunja Mwiko?