Timu ya Taifa ya Kabaddi Tanzania Yaichapa Nigeria Pointi 66-17 India
INDIA — Timu ya Taifa ya Tanzania ya mchezo wa Kabaddi imerejea kwa kishindo katika Mashindano ya Jumuiya ya Madola yanayoendelea nchini India, baada ya kuibuka na ushindi mnono wa pointi 66-17 dhidi ya Nigeria kwenye mechi yao ya pili.
Ushindi huo unakuja kama jibu la haraka baada ya Watanzania hao kuanza mashindano vibaya kwa kupokea kichapo cha pointi 48-21 kutoka kwa Sri Lanka kwenye mchezo wao wa kwanza.
Akizungumza na Soka la Bongo, Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Abass Khamis Suleiman, ameeleza kuwa siri ya ushindi huo mkubwa ilikuwa ni kufanyia kazi makosa yaliyojitokeza kwenye mechi ya kwanza.
“Tumepata pointi hizo baada ya kukaa chini na wachezaji na kurekebisha makosa ambayo yalitugharimu katika mchezo wa kwanza,” alisema Kocha Abass.
Kocha huyo aliongeza kuwa wachezaji walionyesha utulivu na usikivu mkubwa maelekezo yalipotolewa, jambo lililosaidia kupatikana kwa matokeo hayo mazuri. Kwa sasa, timu hiyo inaelekeza nguvu zake zote kwenye mechi zinazofuata ili kuendeleza mfululizo wa ushindi.
Wachezaji Nyota Waliong’ara na Zawadi
Mbali na kupata ushindi huo wa pointi 66-17, Tanzania pia ilitawala tuzo za binafsi za mchezo huo:
-
Hafidh Ali Hamad: Alichaguliwa kuwa Mlinzi Bora wa mchezo (Best Defender).
-
Juma Hamza Sultan: Alinyakua tuzo ya Mshambuliaji Bora (Best Raider).
Pamoja na tuzo hizo, wachezaji hao walijizolea zawadi ya fedha taslimu Rupia 10,000 za India (sawa na takribani Sh277,513 za Kitanzania).