Paula Kajala Afunguka Sababu ya Kumpigania Marioo Mitandaoni
Mwanamitindo na mfanyabiashara mashuhuri nchini, Paula Kajala, amefunguka wazi kuhusu sababu zinazomfanya ashindwe kukaa kimya kila mara mpenzi wake, msanii Marioo (Omary Mwanga), anaposhambuliwa au kuzungumziwa vibaya kwenye mitandao ya kijamii.
Kauli hii ya Paula inakuja mara baada ya kuibuka kwa mzozo wa hivi karibuni ukimhusisha mwanamuziki Ibraah, ambaye alitoa kauli kwenye mitandao zilizotafsiriwa kama kejeli dhidi ya Marioo. Hali hiyo ilimfanya Paula kuingia moja kwa moja kwenye sehemu ya maoni (comment section) kutetea upande wa mpenzi wake.
Akizungumza na chombo cha habari cha Mwanaspoti, Paula alibainisha kuwa kusimama na mpenzi wake wakati wa changamoto ni wajibu wake kama mwenza na mzazi mwenzake.
“Kwangu mimi ni lazima kuingilia ugomvi au changamoto yoyote inayomtokea mpenzi wangu au baba wa mtoto wangu. Sipendi kabisa kumuona akishambuliwa mitandaoni halafu mimi nikakaa kimya,” alisema Paula.
Paula aliongeza kuwa hapendezwi na utamaduni wa watu kudhalilishana mtandaoni, kwani kile kinachochapishwa kinabaki kama kumbukumbu ya kudumu ambayo inaweza kuja kumwathiri hata mtoto wao baadae.
“Sipendi mambo ya kudhalilishana mitandaoni kwa sababu kila kinachowekwa huko kinahifadhiwa. Pia mimi tayari ni mama na nina mtoto, hivyo ni lazima nifikirie mbali kuhusu athari za mambo haya,” alisisitiza.
Kwa msimamo huo, Paula anaamini kuwa kuwa upande wa Marioo wakati wote si tu ni kuonyesha mapenzi, bali ni sehemu ya kuweka heshima na kulinda familia yao dhidi ya mashambulizi ya mtandaoni.