Tuzo za CAF 2026: Winfrida Gerald Aingia Kwenye Orodha ya Wanaowania
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeanza rasmi kutangaza majina ya wanaowania Tuzo za CAF 2026, huku nyota wa soka la wanawake kutoka mataifa mbalimbali wakiongoza orodha ya awali. Katika hatua kubwa kwa soka la Watanzania, mchezaji wa JKT Queens, Winfrida Gerald, amefanikiwa kuingia kwenye orodha hiyo ya dhahabu.
Hafla hiyo ya kutoa tuzo inatarajiwa kufanyika Desemba 7, 2026, jijini Lagos, Nigeria, ambapo mastaa waliofanya vizuri katika kipindi cha tathmini watakutana kupokea heshima zao katika vipengele vya mtu mmoja mmoja, timu za taifa pamoja na klabu.
Kulingana na taarifa iliyotolewa na CAF, orodha ya awali imejumuisha vipengele vinne vya soka la wanawake, huku orodha za vipengele vingine zikisubiriwa kutangazwa rasmi hivi karibuni.
Winfrida Gerald Aiwakilisha Tanzania
Tanzania imepata heshima kubwa baada ya mshambuliaji chipukizi wa JKT Queens, Winfrida Gerald, kutajwa miongoni mwa wanaowania tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi wa Kike Afrika.
Hata hivyo, Winfrida anakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa vipaji vingine vinavyochipukia barani Afrika, vikiwemo:
-
Romaine Gandonou (Benin)
-
Maëva Nyadjou (Cameroon)
-
Grace-Ruth Sery na N’Sira Ouédraogo (Ivory Coast)
-
Rose Kadzere (Malawi)
-
Kautar Azraf (Morocco)
-
Seimeyeha Janet Akekoromowei na Oluwakemi Adegbuyi (Nigeria)
-
Adji Ndiaye (Senegal)
Uteuzi huu ni hatua kubwa kwa soka la wanawake nchini Tanzania, ukionyesha ukuaji wa kiwango cha wachezaji wa ndani katika jukwaa la kimataifa.
Vita ya Mchezaji Bora wa Kike wa Mwaka: Temwa Chawinga Kwenye Charti
Katika kipengele cha Mchezaji Bora wa Kike wa Mwaka, macho ya wengi yelekezwa kwa mshambuliaji hatari wa Malawi, Temwa Chawinga, anayecheza klabu ya Kansas City Current nchini Marekani.
Temwa anakabiliwa na ushindani kutoka kwa dada yake Tabitha Chawinga, Barbra Banda (Zambia), Thembi Kgatlana (Afrika Kusini), pamoja na nyota watatu wa Cameroon: Marie Ngah Manga, Michaely Bihina, na Monique Ngock. Wengine ni Marine Dafeur (Algeria), Portia Boakye (Ghana), na Hanane Aït El Haj (Morocco).
Kinyang’anyiro cha Timu Bora ya Taifa ya Wanawake
Mataifa 10 yaliyotajwa kuwania tuzo ya Timu Bora ya Taifa ya Wanawake ni pamoja na:
-
Algeria
-
Cabo Verde
-
Cameroon
-
Ivory Coast
-
Ghana
-
Malawi
-
Mali
-
Morocco
-
Nigeria
-
Afrika Kusini
Ushindani huu unakuja baada ya mataifa haya kuonyesha kiwango cha juu katika michuano ya AFCON ya Wanawake 2026, ambapo Cameroon ilitwaa ubingwa kwa kuifunga Malawi mabao 3-0 kwenye mechi ya fainali.
Sarr, Gueye na Hakimi Watajwa Tuzo ya Wanaume
Ingawa CAF bado haijatoa orodha rasmi ya wanaowania tuzo ya Mchezaji Bora wa Wanaume, mijadala mikali imetawala kuhusu mastaa waliokuwa na msimu bora.
Majina yanayopewa nafasi kubwa ni pamoja na:
-
Achraf Hakimi na Ismaël Saibari (Morocco)
-
Sadio Mané, Ismaïla Sarr, na Pape Gueye (Senegal)
Ismaïla Sarr na Pape Gueye wamekuwa nguzo muhimu kwa timu ya taifa ya Senegal, huku Gueye akifunga bao la ushindi lililoipa Senegal ubingwa wa AFCON 2025 dhidi ya Morocco.
Makipa na Vijana Chipukizi Wanaowania Heshima
Katika kipengele cha Kipa Bora wa Mwaka, majina kama Yassine Bounou (Morocco), Ronwen Williams (Afrika Kusini), na Vozinha (Cabo Verde) yanatarajiwa kuongoza kinyang’anyiro hicho.
Kwa upande wa Klabu Bora ya Mwaka, klabu ya Al Hilal ya Sudan inatajwa kuwa mwakilishi wa pekee kutoka Kanda ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) anayewania kutikisa katika jukwaa hilo.
Wakati huo huo, tuzo za vijana kwa upande wa wanaume zitawajumuisha wachezaji kama Ibrahim Maza (Algeria), Christian Kofane (Cameroon), Yan Diomandé (Ivory Coast), Ayoub Bouaddi (Morocco), na Ibrahim Mbaye (Senegal).
Lagos Kuwa Kitovu cha Soka Afrika
Tuzo za CAF zinaendelea kuwa miongoni mwa heshima kubwa zaidi katika mchezo wa soka barani Afrika tangu kuanzishwa kwake mwaka 1992. Huku Yaya Touré akishikilia rekodi ya kutwaa tuzo ya wanaume mara nne mfululizo, Asisat Oshoala anashikilia rekodi ya wanawake akiwa ametwaa mara sita.
Desemba 7, 2026, macho yote yatakuwa Lagos, Nigeria, kushuhudia historia mpya ikiandikwa na kuona kama Winfrida Gerald atairejesha tuzo ya chipukizi nchini Tanzania.