Sitaki tena Urais Sehemu ya 19
Burudani

Sitaki tena Urais Sehemu ya 19: Rais Shanga Aagiza Freemason Wote Wakamatwe Usiku!

Vardo November 9, 2026 5:26 pm

Taarifa hizo mpya zilimghadhabisha mno Rais Shanga. Bila kupoteza muda, alimnyanyulia simu Waziri Mkuu na kumtaka afike ofisini kwake mara moja kwa ajili ya kikao cha dharura.

Dakika chache baadaye, Waziri Mkuu alipowasili ofisini hapo, Rais Shanga alimkodolea macho ya hasira na kumuuliza kuhusu agizo lake la awali la kupiga marufuku shughuli zote za kundi la Freemason.

“Unakumbuka vizuri nilikuagiza nini?” Shanga alimhoji kwa sauti ya mamlaka.

“Nilitekeleza agizo lako kwa umakini mkubwa, mheshimiwa,” Waziri Mkuu alijibu kwa unyonge. “Nilihakikisha kuwa usajili wa kundi hilo unafutwa kabisa, na tuliwapelekea barua rasmi ya kuwajulisha kuwa shughuli zao haziruhusiwi tena nchini mwetu.”

“Je, umejidhibitishia kuwa kweli wamesimamisha shughuli zao?”

“Ndiyo, mheshimiwa.”

“Basi taarifa nilizopata hivi karibuni zinasema kundi hilo bado linaendelea na mikutano na shughuli zao kama kawaida!” Rais Shanga alisema kwa kufoka.

“Kama ni hivyo, basi watakuwa wanafanya kosa kubwa la kukiuka sheria na agizo la serikali.”

“Hawa watu wanaonesha ukaidi wa waziwazi!” Rais Shanga aligonga meza na kuendelea, “Sasa ninakuagiza kuhakikisha viongozi wote wa kundi hilo wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria mara moja. Nataka wafundishwa adabu kwa kukiuka agizo la serikali. Umenielewa?”

“Nimekulewa vyema, mheshimiwa Rais.”

“Sasa nenda ukaitekeleze kazi hiyo bila kuchelewa!”

Waziri Mkuu aliporudi ofisini kwake, hakupoteza muda. Alimpigia simu Waziri mpya wa Mambo ya Ndani na kumtaka afike ofisini kwake haraka iwezekanavyo.

Baada ya dakika chache, Waziri wa Mambo ya Ndani alipowasili, Waziri Mkuu alimkabili na maswali: “Siku ile nilikuagiza ufute usajili wa Freemasons na uwaandikie barua ya kupiga marufuku shughuli zao. Je, umefuatilia na kuhakikisha wametii agizo hilo?”

Waziri wa Mambo ya Ndani aliumani mbavu na kujibu, “Kwa kweli sikufuatilia kwa kina, mheshimiwa. Labda nianze sasa hivi kuwatuma vijana wangu wafanye uchunguzi.”

“Mheshimiwa Rais anazo taarifa za uhakika kuwa watu hao wanaendelea na shughuli zao kama kawaida,” Waziri Mkuu alimweleza kwa msisitizo. “Sasa anakutaka uanzishe operesheni maalumu ya kuwakamata viongozi wao wote ili wafikishwe mahakamani.”

“Mheshimiwa, ni vizuri kwanza tupate ushahidi usiotia shaka kabla ya kuwakamata, ili kesi isiingie dosari mahakamani.”

“Rais tayari anazo taarifa kamili na ameagiza wakamatwe!”

“Ili tuwe na ushahidi thabiti wa kuwatia hatiani, ni vyema tufuatilie nyendo zao kwa siri usiku wa leo kabla ya kuwavamia.”

“Utahitaji muda gani kufanya hivyo?” Waziri Mkuu aliuliza.

“Ninachofahamu ni kwamba huwa wanakuwa na mikutano yao siku za Jumamosi na Jumanne usiku. Na leo ni Jumanne! Nitatuma makachero wangu usiku wa leo. Endapo watakuta kuna mkusanyiko, watatiwa baroni papo hapo.”

“Sawa. Fanya hivyo haraka, kisha uniletee taarifa kamili ili niweze kumpatia Mheshimiwa Rais.”

Baada ya kutoka hapo, Waziri wa Mambo ya Ndani alirudi ofisini kwake na kuwaita Mkuu wa Jeshi la Polisi pamoja na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI). Aliwaeleza agizo hilo zito kutoka kwa Rais.

“Wale watu hukutana kila Jumamosi na Jumanne usiku. Je, mnaweza kuwatuma makachero wawili shupavu kwenda kufanya uchunguzi wa siri?” Waziri aliuza.

“Tunaowapata na tutawatuma mara moja,” Mkurugenzi wa Upelelezi alijibu.

“Inatakiwa wasitambulike kabisa. Waingie hadi ndani kabisa ya jumba lao na kujichanya nao kama wanachama wenzao. Tunataka ushahidi usiotia shaka,” Waziri alisisitiza.

Katika kikao hicho, mpango kabambe uliandaliwa wa kuwapenyeza makachero wawili ndani ya jumba hilo lililopo eneo la Osariver. Makachero hao walitakiwa kuvaa suti nyeusi za gharama ili kujichanganya na matajiri hao bila kushukiwa.

Hata hivyo, ili kujikinga na hatari, walikubaliana kuwa endapo makachero hao watagundulika, watajitambulisha na kuwapigia simu polisi wenzao watakaokuwa wanasubiri nje wakiwa na magari mawili ya polisi, askari wenye silaha nzito, na mabomu ya kutoa machozi.

Operesheni hiyo ilihusisha askari polisi kumi na makachero saba wa upelelezi. Makachero wawili walioteuliwa kuingia ndani ya mjengo huo walikuwa Deo na Herman.

Ilipofika saa kumi na moja jioni, upelelezi wa eneo ulianza. Na ilipofika saa moja usiku, magari ya kifahari yalianza kumiminika kwenye geti kuu la jumba hilo la Freemason kama vile wanaingia kwenye klabu ya usiku.

Saa moja na nusu usiku, makachero walitoa taarifa kwa DCI: “Kuna harakati kubwa zinaendelea. Watu wanamiminika ndani.”

“Hicho ndicho tulichotaka kujua. Endeleeni na mpango kama tulivyokubaliana,” DCI aliamuru.

Baada ya maelekezo ya mwisho, Makachero Deo na Herman walipanda gari la kawaida la kiraia na kuelekea Osariver.

Ilipofika saa mbili na dakika moja usiku, Herman aliliingiza gari lao langoni mara tu baada ya gari lingine kufunguliwa geti. Hawakujua kuwa kila gari lililoingia lilikuwa likinaswa na kamera za ulinzi zilizokuwa zikifuatiliwa kwenye chumba maalumu cha ulinzi.

Walipoingia ndani ya ukumbi, walikuta waumini na wanachama wengi wakiwa wameketi kimya. Osaka aliingia na kuanza kuongoza ibada hiyo ya siri.

Mara ghafla, kivuli cha mtu aliyeketi kilitokea kwenye kioo kikubwa kilichopo mbele ya ukumbi. Sauti nzito na ya kutisha ilisikika kutoka kwenye kioo hicho ikimlaani vikali Rais Shanga:

“Sisi ndio tuliomweka madarakani kwa makubaliano maalumu ambayo sasa ameyageuka! Lakini paka hashindwi na utumbo wake! Tutapambana na utawala wake hadi mwisho!”

Deo na Herman walitazamana kwa wasiwasi mkubwa. Lakini kabla hawajamaza kutafakari maneno hayo, sauti ile nzito kutoka kwenye kioo ilinguruma tena kwa msisitizo uliowafanya miili yao isisimke:

“Leo hii, kuna sura mbili ngeni miongoni mwetu. Tungependa watu hao wanaojua wazi kuwa hawatakiwi kuwa humu ndani, wafike hapa mbele mara moja!”

Je, Deo na Herman watapona katika mtego huu mzito? Usikose Sehemu ya 20 kesho hapa Hapa

Simba Yafunguka: Ukweli Kuhusu Deni la Kocha Davids Fadlu Meridianbet Yakupa Sababu Zaidi Ya Kubashiri Kupitia Bet Boost