Simba Yapewa Masharti Makali ya CAF Uwanja wa Uhuru | CAFCL
Klabu ya Simba SC imepata ruhusa kutoka kwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kutumia Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mechi zake za nyumbani za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL), lakini ikikabiliwa na kizuizi cha idadi ya mashabiki.
Akizungumzia hatua hiyo, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amethibitisha kuwa klabu imeipokea taarifa hiyo kwa furaha kubwa, kwani inatoa uhakika wa kituo chao cha nyumbani kwenye mashindano hayo makubwa barani Afrika.
Hata hivyo, Ahmed alibainisha kuwa ruhusa hiyo kutoka CAF imekuja na masharti mepesi ya miundombinu pamoja na udhibiti mkali wa idadi ya mashabiki watakaoruhusiwa kuingia uwanjani.
“Kwa mujibu wa viwango na tathmini ya CAF, Uwanja wa Uhuru una uwezo wa kubeba mashabiki 19,000. Lakini kwa mechi zetu za hatua ya makundi, uwanja huo umeruhusiwa kuingiza mashabiki 6,000 pekee,” alisema Ahmed Ally.
Licha ya kuzuiliwa kwa idadi hiyo ya mashabiki, uongozi wa Simba umeeleza kuwa sasa akili zote ziko kwenye maandalizi ya mikikimikiki ya hatua hiyo ili kuhakikisha wanapata matokeo chanya nyumbani.
Ahmed amewatoa hofu mashabiki kwa kueleza kuwa klabu itatoa utaratibu rasmi na wa wazi utakaotumika kugawa nafasi hizo 6,000 ili kuwapa fursa wanasimba kupata tiketi za kushuhudia mechi hizo za Ligi ya Mabingwa Afrika.