Mlandege FC Kombe la FA
Michezo Bongo

Hat-Trick ya Kivelege Yaipeleka Mlandege 16 Bora Kombe la FA, Atuma Onyo kwa Fufuni SC

Vardo November 13, 2026 5:44 pm

Mshambuliaji wa klabu ya Mlandege FC, Boniphace Nickson Kivelege, ameonyesha furaha yake kubwa baada ya kuiongoza timu yake kutinga hatua ya 16 bora ya michuano ya Kombe la FA kufuatia ushindi mnono wa mabao 5-2 dhidi ya Urafiki SC.

Katika mchezo huo mkali wa hatua ya 32 bora uliopigwa kwenye Uwanja wa Mao A, Unguja, Kivelege aliibuka shujaa na nyota wa mchezo baada ya kufunga mabao matatu peke yake (hat-trick) yaliyoihakikishia Mlandege tiketi ya kusonga mbele.

Akizungumza mara baada ya filimbi ya mwisho, Kivelege amesema ushindi huo ni hatua muhimu katika kutimiza malengo ya klabu msimu huu, akisisitiza kuwa wamejipanga kupambana hadi mwisho ili kutwaa taji hilo.

“Furaha yangu ni kuona tumefuzu hatua inayofuata. Tunafahamu umuhimu wa michuano hii, hivyo tutahakikisha tunafanya vizuri katika kila hatua ili kutimiza malengo yetu. Nimefurahi pia kufunga mabao matatu na kuisaidia timu kupata ushindi,” amesema Kivelege.

Nyota huyo ameongeza kuwa jukumu lake kuu kama mshambuliaji ni kufunga mabao, hivyo hujisikia fahari kila anapoitendea haki jezi ya Mlandege FC kwa kuipa matokeo chanya.

Hata hivyo, Kivelege amebainisha kuwa kwa sasa wameweka kando shangwe za Kombe la FA na kuelekeza nguvu zote kwenye mchezo ujao wa Ligi Kuu dhidi ya Fufuni SC, utakaochezwa siku ya Jumapili katika Uwanja wa Mao A kuanzia saa 10:00 jioni.

Beach Penalties Kutoa Burudani Ya Soka Na Ufukweni Kwa Kila Kifaa Uwanja wa Mao Zedong Waingiza Sh47.4 Milioni Ndani ya Miezi Mitatu Zanzibar!