Rasmi: Kinda wa Simba SC Bakari Msimu Arejea Mazoezini Baada ya Majaribio SKN St. Pölten ya Austria
KINDA machachari wa klabu ya Simba SC, Bakari Msimu, amerejea rasmi nchini na kuungana na wenzake katika mazoezi ya kikosi hicho baada ya kukamilisha majaribio ya siku tano nchini Austria.
Msimu aliwasili nchini usiku wa kuamkia leo akitokea Austria, ambako alikuwa kwenye klabu ya SKN St. Pölten inayoshiriki ligi za nchini humo kwa ajili ya kuonyesha kipaji chake ili kuangalia uwezekano wa kusajiliwa na kucheza soka la kulipwa barani Ulaya.
Kinda huyo aliondoka nchini akiwa na matumaini makubwa ya kuwashawishi viongozi na benchi la ufundi la SKN St. Pölten ili kupata nafasi ya kujiunga nao na kufungua milango mipya ya mafanikio nje ya Tanzania.
Mara baada ya kukamilisha programu hiyo ya majaribio ya siku tano, nyota huyo amerejea moja kwa moja katika kambi ya Wekundu wa Msimbazi na kuanza kujifua chini ya usimamizi wa benchi la ufundi la timu hiyo.
Hata hivyo, pamoja na kurejea kwake nchini, hatima ya usajili wake nchini Austria bado haijafahamika rasmi. Msimu sasa anasubiri ripoti na majibu kutoka kwa uongozi wa SKN St. Pölten yatakayotoa tathmini ya kiwango alichokionyesha wakati wote wa majaribio hayo.
Kwa sasa, Bakari Msimu ataendelea na majukumu yake ndani ya kikosi cha Simba SC huku akisubiri taarifa hiyo itakayoamua iwapo atapata nafasi ya kutimkia Austria au ataendelea kuitumikia klabu yake ya sasa.