Uchaguzi Simba SC
Simba SC

Mzee wa Salute na Vigogo Wengine Wajitosa Uchaguzi wa Simba SC, Wataja Sababu za Kuchukua Fomu

Vardo November 19, 2026 12:04 am

Mchakato wa kuelekea Uchaguzi Simba SC umezidi kushika kasi baada ya mwanachama maarufu wa klabu hiyo, Hassan Bakari Kakayoo maarufu kama ‘Mzee wa Salute’, kujitokeza na kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya ujumbe wa Bodi ya Wakurugenzi.

Kakayoo alichukua fomu hiyo jana, Novemba 18, 2026, katika makao makuu ya klabu hiyo na kuungana na wanachama wengine walioonyesha nia ya kuongoza wekundu hao wa Msimbazi.

Akizungumza mara baada ya kukamilisha hatua hiyo, Mzee wa Salute alimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kufika salama na kusisitiza kuwa uamuzi wake unatokana na haki yake ya kikatiba ndani ya klabu.

“Nimechukua fomu hii kwa sababu ni haki yangu ya msingi ya kikatiba. Hata hivyo, kutokana na miongozo na taratibu za uchaguzi, kuna mambo mengi ambayo kwa sasa siwezi kuyazungumzia hadharani,” alisema Kakayoo.

Hii si mara ya kwanza kwa kada huyo kujitosa kwenye kinyang’anyiro hicho, kwani aliwahi pia kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyohiyo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.

Sura Nyingine Zilizojitokeza

Mbali na Kakayoo, wanachama wengine wawili walifika ofisini hapo kuchukua fomu za kuwania ujumbe wa Bodi ya Wakurugenzi hadi kufikia saa 10:00 jioni:

  • Wilfred Nyamwija: Amejitosa rasmi kwenye kinyang’anyiro hicho kuwania nafasi ya ujumbe wa bodi.

  • Salum Hamidu: Makamu Mwenyekiti wa Matawi ya Simba Mkoa wa Dar es Salaam, ambaye alichukua fomu yake kimyakimya bila kuzungumza na waandishi wa habari.

Tofauti na siku za awali ambazo zilishuhudia idadi kubwa ya vigogo wakimiminika kuchukua fomu, jana idadi ya waliojitokeza ilikuwa ndogo ambapo ni wanachama hao watatu pekee waliofika ofisini.

Tarehe Mpya ya Uchaguzi Mkuu wa Simba

Kwa mujibu wa ratiba ya sasa, uchaguzi huo mkuu wa Klabu ya Simba unatarajiwa kufanyika Januari 30, 2027, baada ya kusogezwa mbele kutoka tarehe ya awali ya Januari 3. Viongozi watakaochaguliwa watachukua kijiti cha kuiongoza klabu hiyo kutoka kwa uongozi unaomaliza muda wake chini ya Mwenyekiti, Murtaza Ally Mangungu.

Matokeo: Simba Queens Yabanwa Mbavu na Ceasiaa Queens Nyumbani!