Simba vs Orlando Pirates Novemba 29: Ahmed Ally Afunguka Kipimo cha JKT Tanzania!
Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu ya Simba SC, Ahmed Ally, amesema mchezo wao dhidi ya JKT Tanzania umewapa kipimo sahihi na picha halisi ya ushindani wanaoutarajia katika pambano la Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini, litakalopigwa Novemba 29, 2026.
Akizungumza mara baada ya mchezo huo, Ahmed amebainisha kuwa licha ya utofauti wa viwango kati ya Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, mchezo huo umewasaidia kujitathmini, kubaini maeneo ya kuboresha, na kuweka mipango imara zaidi kabla ya kuvaana na wapinzani hao wa kimataifa.
JKT Tanzania Yapongezwa kwa Kasi na Ushindani
Ahmed ameisifu JKT Tanzania kwa kuingia uwanjani kwa ujasiri, kucheza kwa kasi, na kutojifungia nyuma, hali iliyoufanya mchezo kuwa na ushindani mkali kuanzia mwanzo hadi mwisho.
“Level ya ligi, japo hawajafikia level ya Ligi ya Mabingwa, lakini angalau umepata mchezo ambao kwanza unakuonyesha wewe uko wapi, lakini unautumia mchezo huu kujipanga. Mchezo huu wa leo ulikuwa na intensity kubwa, hakuna hata dakika moja ambayo JKT walikaa kurinda. Hili lazima tuwapongeze JKT kwa kutaka kupishana na kubishana na Simba. Kwa hiyo hiyo ndiyo Ligi ya Mabingwa na mchezo wa leo tumepata ladha halisi ya mechi yetu kuelekea mchezo dhidi ya Orlando tarehe 29 ya mwezi huu,” amesema Ahmed.
Ushindi Wapandisha Morali Kuelekea Mechi ya Kimataifa
Mbali na kupima kiwango cha kikosi, Ahmed amesema ushindi dhidi ya JKT Tanzania umeongeza kujiamini kwa wachezaji na kuchochea hamasa kubwa kwa mashabiki kuelekea mchezo wa Simba vs Orlando Pirates.
Ameongeza kuwa matokeo chanya kwenye mechi za ndani yana mchango mkubwa katika kuandaa saikolojia ya timu kabla ya mechi za kimataifa, akisisitiza kuwa kupoteza au kutoka sare kunaweza kushusha morali ya wachezaji na mashabiki.
“Tumewafunga JKT lakini vilevile tumepata kipimo kizuri na confidence, kwa sababu unapoenda kwenye Ligi ya Mabingwa wakati mechi ya ndani umepoteza ama umepata sare inakuwa inakudhoofisha, inashusha morali ya mashabiki wako. Kwa hiyo hata shabiki anajiuliza kama tumefungwa na JKT, tutawezaje kwenda kufunga Orlando? Kwa hiyo ukipata ushindi, mara nyingi unaingia katika mchezo na Orlando mkiwa na confidence ya kutosha kweli kweli,” amesisitiza.
Kwa sasa, Simba SC inaendelea na maandalizi kuelekea mchezo huo wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ikilenga kutumia ushindi na kasi iliyoonyesha dhidi ya JKT Tanzania kama chachu ya kupata matokeo mazuri mbele ya Orlando Pirates