Barker Atuma Salamu Nzito Orlando Pirates: “Simba Tumejipanga Kuwaonyesha Kazi”
KOCHA Mkuu wa Simba, Steve Barker, ametuma salamu nzito kwa wapinzani wao Orlando Pirates ya Afrika Kusini, akisisitiza kuwa kikosi chake kimejipanga kikamilifu kuibuka na ushindi katika mchezo wao wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika utakaopigwa Jumapili hii.
Mtanange huo mkali wa Simba vs Orlando Pirates unatarajiwa kurindima kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam, ambapo Wekundu wa Msimbazi wanalenga kuanza kampeni yao ya makundi kwa kishindo mbele ya mashabiki wao.
Akizungumza kuelekea mchezo huo, Barker amebainisha kuwa mafanikio kwenye michuano mikubwa ya CAF yanahitaji kujituma kwa hali ya juu, huku akiweka wazi kuwa kiu ya ushindi imetawala kuanzia ngazi ya uongozi hadi kwa wachezaji.
“Tuna matamanio makubwa ya kufanikiwa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini hilo linahitaji kujituma na kupambana ili kufanya vizuri. Haya ndiyo matamanio ya wote, kuanzia uongozi, wachezaji na kila mmoja anayeipenda Simba,” amesema Barker.
Ukubwa wa Orlando Pirates Hauwatishi Simba SC
Pamoja na kutambua historia na ubora wa Orlando Pirates katika ramani ya soka la Afrika, kocha huyo raia wa Afrika Kusini amesisitiza kuwa hilo halitawazuia vijana wake kupambana kufa na kupona kusaka alama tatu muhimu nyumbani.
“Tunacheza na moja ya timu kubwa Afrika, Orlando Pirates, na tunalitambua hilo. Lakini kwa pamoja tumejipanga kuhakikisha tunafanya vizuri katika mchezo wa Jumapili,” ameongeza kocha huyo.
Ushindi katika mchezo huu wa ufunguzi utakuwa na maana kubwa kwa Simba SC katika kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kufuzu hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.