Senegal warejeshewa ubingwa wa AFCON
Habari za michezo

RASMI: CAS Yawarejeshea Senegal Ubingwa wa AFCON 2025, Morocco Wapokonywa Kombe!

Vardo November 24, 2026 7:37 pm

Timu ya Taifa ya Senegal imerejeshewa rasmi ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025) baada ya Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) kutengua uamuzi wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) uliokuwa umeipokonya taji hilo na kulikabidhi kwa Morocco.

Uamuzi huo wa kihistoria umetolewa leo, Novemba 24, 2026, kufuatia rufaa iliyowasilishwa na Shirikisho la Soka la Senegal (FSF), wakipinga adhabu ya CAF iliyotangaza Morocco kuwa mabingwa kwa ushindi wa mezani wa mabao 3-0.

Chanzo cha Mgogoro wa Fainali ya AFCON 2025

Awali, Senegal ilitwaa ubingwa huo uwanjani kwa kuifunga Morocco bao 1-0 katika mchezo wa fainali uliochezwa Januari 18, 2026, jijini Rabat, Morocco. Bao pekee la ushindi lilifungwa na kiungo Pape Gueye katika dakika za nyongeza.

Hata hivyo, fainali hiyo iliingia kwenye utata mkubwa baada ya wachezaji wa Senegal kugoma na kuondoka uwanjani kwa takribani dakika 15, wakipinga uamuzi wa mwamuzi wa kutoa penalti kwa Morocco katika dakika za lala salama. Baada ya mchezo kurejea, penalti hiyo iliyopigwa na Brahim Diaz iliokolewa, kabla ya Senegal kupata bao la ushindi.

Uamuzi wa CAF na Rufaa ya CAS

Mnamo Machi 17, 2026, Kamati ya Rufaa ya CAF ilibatilisha matokeo ya uwanjani na kuitangaza Senegal kuwa imepoteza mchezo huo kwa mujibu wa kanuni za mashindano, huku Morocco ikipewa ushindi wa mezani wa mabao 3-0.

Hatua hiyo iliisukuma FSF kukata rufaa katika mahakama ya CAS, ambayo sasa imerejesha matokeo halali ya uwanjani na kuithibitisha Senegal kuwa ndiyo mabingwa rasmi wa Afrika. Kwa kuwa hakuna chombo kingine cha juu cha kukata rufaa zaidi ya CAS, sakata hili limefungwa rasmi.

Yanga Yatangaza Viingilio vya Mechi Dhidi ya MC Alger Zanzibar – Hii Hapa Orodha Kamili! Ismail Mgunda Afunguka Mazito Simba, Ataja Siri ya Ushindani Wake na Elie Mpanzu