Libasse Gueye Awavaa Mashabiki Simba: “Acheni Kumcheka Ibrahim Doumbia, Mpeni Muda!”
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Simba SC, Libasse Gueye, amewataka mashabiki na wadau wa soka nchini kuacha mara moja tabia ya kumkosoa na kumfanyia mzaha kiungo mwenzake, Ibrahim Doumbia, kupitia mitandao ya kijamii, akisisitiza kuwa mchezaji huyo anahitaji muda na kutiwa moyo.
Akizungumza kuhusu mwenendo wa kiungo huyo tangu ajiunge na kikosi cha Wekundu wa Msimbazi, Libasse Gueye amebainisha kuwa kejeli zinazoendelea dhidi ya Ibrahim Doumbia zimevuka mipaka na zinaweza kuathiri saikolojia na kiwango chake uwanjani.
Gueye amefafanua kuwa ingawa mwanzoni utani wa mitandaoni ulionekana kama jambo la kawaida la kimichezo, kwa sasa hali hiyo imekuwa kubwa kupita kiasi na inamnyima mchezaji huyo uhuru wa kuonyesha uwezo wake halisi.
“Doumbia bado ni kijana, anahitaji motisha na kutiwa moyo. Mwanzoni alipokuja ilikuwa ni jambo la kuchekesha kum-post na mambo mengine, lakini sasa imekuwa nyingi mno kwake. Inabidi tumwelewe, kwa sababu ni binadamu kama wengine,” amesema Gueye.
Aidha, nyota huyo amewaomba mashabiki wa Simba kumpa nafasi Doumbia atulie na kuzoea mazingira mapya ya soka la Tanzania badala ya kumuwekea presha isiyo ya lazima.
Gueye amehitimisha kwa kueleza imani yake kuwa endapo kiungo huyo ataachwa afanye kazi yake kwa utulivu, ataimarika hatua kwa hatua na kuwa msaada mkubwa katika kikosi cha Simba kwenye mashindano yote yanayowakabili.