Simba Waweka Kambi ya Siri Kuikabili Orlando Pirates Jumapili
Kikosi cha wekundu wa Msimbazi, Simba SC, kinatarajia kuingia kambini rasmi leo Jumatano jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa kusisimua wa Simba dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini. Mchezo huo wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF Champions League) utapigwa Jumapili hii katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amebainisha kuwa uongozi umeamua kubadili eneo la kambi kutoka lile walilolizoea ili kuwapa wachezaji utulivu wa hali ya juu na umakini kuelekea mtanange huo mgumu.
“Leo Jumatano tunatarajia rasmi kuingia kambini kwa ajili ya kujiandaa na mechi yetu dhidi ya Orlando Pirates. Kambi yetu tutaiweka mbali kidogo na eneo ambalo tumezoea, ili vijana wapate sehemu tulivu na nafasi ya kufanya maandalizi makubwa kuelekea mchezo huo,” amesema Ahmed Ally.
Ujio wa Orlando Pirates Nchini Bado Kitendawili
Katika hatua nyingine, Ahmed Ally amefichua kuwa hadi sasa klabu hiyo haijapokea taarifa rasmi kutoka kwa wapinzani wao juu ya siku na muda watakaowasili nchini Tanzania, licha ya kufanya jitihada za kuwasiliana nao.
Ameeleza kuwa huenda kuchelewa huko kunatokana na Orlando Pirates kuwa na majukumu ya mchezo wa ligi nchini kwao Afrika Kusini leo, kabla ya kuanza safari ya kuja Dar es Salaam.
“Mpaka sasa bado hatujapokea taarifa rasmi kutoka kwa wapinzani wetu kuhusu wanaingia lini. Tumejaribu kuzungumza nao lakini bado hawajatupa taarifa. Pengine kwa sababu wana mchezo leo Afrika Kusini, wakimaliza watatueleza ratiba yao nzima ya kuja ili na sisi tuweze kuandaa yale tunayopaswa kuwaandalia kwa mujibu wa kanuni,” ameongeza Ahmed.
Malengo ya Simba Nyumbani
Simba inaingia katika mchezo huo ikiwa na dhamira moja tu ya kutumia vyema faida ya uwanja wa nyumbani na mashabiki wake kuvuna pointi tatu muhimu zitakazoiweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa kundi lao.