Dickson Job Afunguka Baada ya Kipigo cha MC Alger: “Kila Mechi Sasa ni Fainali”
Nahodha Msaidizi wa klabu ya Yanga SC, Dickson Job, amewataka wachezaji wenzake kusahau matokeo mabaya ya mchezo wa ufunguzi na kuelekeza nguvu zote katika michezo inayofuata ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF Champions League).
Kauli hiyo ya Dickson Job imekuja muda mfupi baada ya mabingwa hao wa Tanzania kukubali kichapo cha bao 1-0 dhidi ya MC Alger ya Algeria, katika mchezo wa Kundi B uliopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar. Yanga ilipoteza alama tatu muhimu nyumbani baada ya kuruhusu bao la dakika za lala salama kupitia mpira wa adhabu ndogo (set piece), licha ya kutawala sehemu kubwa ya mchezo na kutengeneza nafasi kadhaa za wazi.
Ulinzi Imara wa MC Alger na Kukosa Umakini
Akizungumzia mwenendo wa mchezo huo, beki huyo kisiki amekiri kuwa kikosi chao kilipambana kutafuta mabao, lakini safu ya ulinzi ya MC Alger ilikuwa imara kuzima mashambulizi yao. Hata hivyo, amebainisha kuwa kupoteza umakini katika dakika za mwisho ndiko kulikoigharimu timu.
“Jukumu letu kubwa sasa ni kuinua vichwa na kuangalia maeneo gani tunahitaji kufanya vizuri zaidi. Tunapaswa kuwa makini katika michezo inayofuata ili kuhakikisha tunapata matokeo mazuri,” amesema Job.
Kipigo Kimekuwa Funzo kwa Kikosi
Job ameongeza kuwa ingawa kuanza hatua ya makundi kwa kupoteza nyumbani hakukuwa kwenye mipango yao, matokeo hayo yamewaamsha na kuwapa somo muhimu la kurekebisha makosa yao kabla ya kushuka tena dimbani.
“Matokeo ya kupoteza mchezo wa kwanza hayajaleta taswira nzuri, lakini yametustua na kutufanya tutambue kuwa tunahitaji kuinua vichwa vyetu na kuangalia tunakokwenda,” amesisitiza nahodha huyo msaidizi.
Kila Mchezo Sasa ni Fainali
Kwa kumalizia, Dickson Job amewahakikishia mashabiki wa Yanga kuwa hawana muda wa kuendelea kujutia matokeo yaliyopita, akisisitiza kuwa michezo yote iliyosalia kwenye Kundi B wataichukulia kama fainali ili kutimiza lengo la kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo mikubwa barani Afrika.