ANAITWA Junior Lukosa raia wa Nigeria anatajwa kuingia kwenye rada za Simba kwa ajili ya michuano ya kimataifa kwa kuwa Simba inashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa hatua ya makundi.
Licha ya dirisha la usajili wa Bongo kufungwa Januari 16 bado Simba ina nafasi za kusajili kwa mujibu wa Caf ila wachezaji hawa watatumika kwenye Ligi ya Mabingwa pekee.
Junior ana uzoefu wa kucheza soka la Afrika ikiwa amecheza ndani ya Klabu ya Esperance ya Tunis, Kano Pillars ya Nigeria na alikuwa anacheka na nyavu tu.
Ana umri wa miaka 27 ana uwezo wa kucheka na nyavu ambapo akiwa na First Bank pia alikuwa anafunga kila anapopata nafasi ya kufanya hivyo.
Akiwa na Pillars aliweza kutupia jumla ya mabao 19 ilikuwa msimu wa 2018/19 na ana tuzo ya mfungaji bora baada ya kucheza zaidi ya mechi 20.
Ndani ya Klabu ya Esperance ya Tunis alipata nafasi ya kucheza mechi 11 za mashindano sita na Ligi ya Mabingwa Afrika alicheza mechi nne.
Inaelezwa kuwa Klabu ya Simba inahitaji saini ya nyota huyo ili aweze kuongeza nguvu kwa kikosi hicho ambacho kwa sasa kipo chini ya Kaimu Kocha Mkuu, Seleman Matola.