KOCHA mkuu wa klabu ya Simba, Didier Gomes Da Rosa amefunguka kuwa anataka kuona kikosi chake kinatwaa makombe katika michuano yote wanayoshiriki, na kwa kuanzia wataanza na kombe la michuano ya Simba Super Cup.
Simba ilianza vizuri kibarua chake cha michuano ya Simba Super Cup baada ya kuibamiza Al Hilal ya Sudani kwa mabao 4-1 kwenye mchezo wa ufunguzi wa michuano hiyo iliyo na dhumuni la kuziandaa timu shiriki kuelekea michezo ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Gomez alitangazwa rasmi kuwa kocha mkuu wa klabu ya Simba Jumapili ya Januari 24 akichukua nafasi iliyoachwa na Mbelgiji, Sven Vandenbroeck ambaye alijiuzulu nafasi hiyo Januari 7, na kocha huyo mpya tayari amesimamia mazoezi ya kikosi chake kwa siku nne mfululizo.
Michuano ya Simba Super Cup iliyoanza jana inashirikisha timu tatu ambazo ni Al Hilal, TP Mazembe na mwenyeji Simba.
Akizungumzia malengo ya Simba katika michuano hiyo Gomez amesema: “Kwangu kila mchezo nauchukulia kama fainali hivyo ni lazima tupambane kuhakikisha tunalichukua kombe hili.
“Hii itatujengea hali ya kujiamini na hamu ya kushinda makombe mengine katika michuano tunayoshiriki,”