CEDRIC Kaze,Kocha Mkuu wa Yanga amesema kuwa malengo yao ya kusaka ubingwa wa Ligi Kuu Bara yapo palepale,licha ya uwepo wa watu ambao wanawakatisha tamaa.
Jana, Februari 13 Yanga ikiwa Uwanja wa Sokoine Mbeya, ililazimisha sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Mbeya City na kugawana pointi mojamoja.
Yanga ilianza kupachika bao la kuongoza kupitia kwa Deus Kaseke ambaye akitokea benchi kipindi cha pili akichukua nafasi ya Farid Mussa kwa bao ambalo lilikuwa na utata dakika ya 84.
Bao hilo lilifungwa huku alionekana kwamba mchezaji wa Mbeya City aliokoa kabla mpira haujavuka mstari huku lile la Mbeya City likifungwa kwa penalti na Athanas Pastory dakika ya 90+1.
Kaze amesema:”Kuna watu ambao wanatulatisha tamaa kuelekea safari yetu ya kusaka ubingwa ila hatujakata tamaa tutaendelea kupambana.
“Wachezaji wanajituma na juhudi inaonekana hivyo wakati ujao tutafanya vizuri zaidi,mashabiki watupe sapoti bila kuchoka,”.
Sare ya Yanga inawafanya wafikishe jumla ya pointi 45 wakiwa nafasi ya kwanza. Fiston Abdulazack ingizo jipya ndani ya Yanga alianza jana kwa mara ya Kwanza kutumika ndani ya Ligi Kuu Bara.