FISTON Abdoul Razack, mshambuliaji mpya ndani ya kikosi cha Yanga amesema kuwa anaamini atafanya kazi yake ya kufunga mabao kwa ushirikiano na wachezaji wenzake ndani ya timu hiyo.
Nyota huyo ni ingizo jipya kwenye dirisha dogo ambapo alisaini dili la miezi sita akitokea Klabu ya ENPPI ya Misri na anatajwa kuwa mtatuzi wa tatizo la ubutu wa safu ya ushambuliaji wa Yanga.
Safu ya Yanga kwa upande wa ushambuliaji inaongozwa na Deus Kaseke mwenye mabao matano na ana pasi moja huku nyota Michael Sarpong na Yacouba Songne wakiwa wametupia mabao mannemanne.
Ikiwa imecheza jumla ya mechi 19 imefunga jumla ya mabao 30 na imefungwa mabao nane, ipo nafasi ya kwanza na pointi zake kibindoni ni 45.
Imewaacha kwa pointi sita watani zake wa jadi, Simba ambao wapo nafasi ya pili na pointi 39 baada ya kucheza mechi 17.
Fiston tayari amecheza mechi moja ya Ligi Kuu Bara ilikuwa mbele ya Mbeya City kwenye sare ya kufungana bao 1-1 na pia amecheza mchezo mmoja wa kirafiki ilikuwa wakati Yanga ikipoteza kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya African Sports ya Tanga.
Nyota huyo amesema:”Nimeona wachezaji ni wazuri na wanapenda kupata matokeo ndani ya uwanja hivyo nami nitashirikiana nao kupata matokeo chanya na kufunga mabao pale ambapo ninapata nafasi.
“Ushindani ni mkubwa na kila timu inahitaji kupata matokeo chanya ndani ya uwanja, bado tuna muda wa kufanya vizuri na mashabiki watapenda wenyewe,” amesema.
Kesho Febbruari 17, Yanga itakuwa na kibarua cha kusaka pointi tatu mbele ya Kagera Sugar ya Mecky Maxime iliyo nafasi ya 10 na pointi 23, Uwanja wa Mkapa.
Mchezo wa kwanza walipokutana Uwanja wa Kaitaba, Kagera Sugar ilipoteza kwa kufungwa bao 1-0 hivyo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.