MWAMUZI Ludovic Charles ambaye alichezesha mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya Mbeya City na Yanga, Uwanja wa Sokoine kwenye sare ya kufungana bao 1-1 jina lake ni miongoni mwa waamuzi ambao watajadiliwa na Kamati ya Waamuzi hivi karibuni ili kuweza kufanya tathimini ya kile ambacho alikifanya.
Mwamuzi huyo alionekana kulalamikiwa na wachezaji wa timu zote mbili kwa kuyakubali mabao mawili ambayo yalikuwa na utata na baada ya kumaliza mchezo wachezaji wa Yanga walionekana kumfuata tena jambo lililofanya atoke chini ya ulinzi huku nahodha Lamine Moro akiwatuliza wachezaji wake.
Miongoni mwa mambo ambayo yalionekana kulalamikiwa ndani ya Uwanja wa Sokoine ni pamoja na tukio la fair play dakika ya 25, Mbeya City walikuwa kwenye umiliki wa mpira ila mwamuzi alisimamisha mpira kwa kile alichodai kuwa kuna mchezaji wa Yanga amechezewa faulo.
Dakika ya 67 Deus Kaseke baada ya kuingia akichukua nafasi ya Farid Mussa aliweza kubadili mchezo na Kaseke alionekana kuchezewa faulo ndani ya 18 dakika ya 77 na mchezaji wa Mbeya City.
Tukio hilo mwamuzi alipeta na kuruhusu Mbeya City waendelee na mchezo ndani ya Uwanja wa Sokoine jambo ambalo lililamikiwa na wachezaji.
Bao la Kaseke wa Yanga, alifunga dakika ya 84 na lilionekana kuwa na utata kwa kuwa mchezaji mmoja wa Mbeya City alionekana akiokoa mpira ule kabla ya kuvuka mstari.Tukio hilo lilisababisha wachezaji wa Mbeya City kumlalamikia na kipa namba moja Haroun Mandanda alionyeshwa kadi ya njano.
Penalti ya Yanga iliyotolewa na Lodovic dakika ya 90 baada ya Yassin Mustapha kufuatwa na mpira wakati akiruka ndani ya 18 ililalamikiwa na wachezaji wa Yanga na ilisababisha kadi ya njano kwa nahodha Lamine Moro.Penalti hiyo ilifungwa na Pastory Athanas.
Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi Tanzania, Sud Abdi Mohammed alisema kuwa hawezi kuzungumzia maamuzi ya kwenye mchezo huo wa Mbeya City na Yanga kwa kuwa ipo kamati inayoshughulikia makosa.
“Ukitaka nizungumzie maamuzi ya mchezo wa Mbeya City na Yanga huo kwa sasa sitaweza kuzungumzia kwa kuwa ipo kamati maalumu ambayo huwa inakaa kujadili masuala yanayohusu maamuzi.
“Ikiwa nitasema nizungumzie jambo hilo ninaweza kuonekana ninamtetea ama kumkandamiza hivyo hilo tuachie kamati itafanya kazi yake.
“Ila kabla ya mzunguko wa pili kuanza tulitoa mafunzo ya vitendo na nadharia kwa muda wa siku tano ambapo tulianza Januari 29 mpaka Februari 2 kwa waamuzi wa Ligi Kuu na tuliwapeleka uwanjani na darasani na tuliwaambia wazingatie sheria na kuchezesha kwa umakini,” amesema.
Cedric Kaze, Kocha Mkuu wa Yanga amesema kuwa alishangazwa na maamuzi wa mchezo huo jambo ambalo hakulitarajia.
Mathias Lule, Kocha Mkuu wa Mbeya City amesema kuwa kuhusu mwamuzi kuamua bao lile hana cha kufanya kwa kuwa hawezi kubadilisha maamuzi yake.