Home Yanga SC MAXIME:HAIKUWA SHUGHULI NDOGO, FEI ATOKWA NA MACHOZI

MAXIME:HAIKUWA SHUGHULI NDOGO, FEI ATOKWA NA MACHOZI


 MECKY Maxime, Kocha Mkuu wa Kagera Sugar amesema kuwa haikuwa shughuli ya kitoto kwa timu yake kulazimisha sare ya kufungana mabao 3-3 dhidi ya Yanga jana Februari 17.

Ikiwa ugenini ilikubali sare hiyo ambapo mabao ya Kagera Sugar yalifungwa na Peter Mwalyanzi dakika ya 10,Hassan Mwaterema dakika ya 23 na Yusuph Mhilu dakika ya 45+1.

Yale ya Yanga inayonolewa na Cedric Kaze yalifungwa na Tuisila Kisinda kwa mkwaju wa penalti dakika ya 13, Deus Kaseke dakika ya 29 na Tonombe Mukoko dakika ya 60.

Matokeo hayo yanaifanya Kagera Sugar kwenye msimamo kufikisha jumla ya pointi 24 ikiwa nafasi ya 9 huku Yanga ikiwa nafasi ya kwanza na pointi zake 46 zote zimecheza jumla ya mechi 20.

Kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Kaitaba, Kagera Sugar ilipoteza kwa kufungwa bao 1-0 na kuyeyusha pointi tatu mazima nyumbani ila jana iliambulia pointi moja.

Maxime amesema:”Haikuwa shughuli ya kitoto, kazi ilikuwa kubwa, kwa jambo hilo ninawapongeza wachezaji wangu kwa kuwa walicheza kwa jitihada kusaka pointi tatu ndani ya uwanja ila wakaambulia moja.

“Unajua mpira ni burudani na mabao,sasa nilipoona tumepata bao la kwanza nikawaambia vijana chezeni, sasa tulipofungwa bao la kusawazisha nikawaruhusu wacheze tena tukafunga.

“Jamaa wakatufunga tena tukarudi na burudani ikaendelea hivyo hamna namna nimewapongeza wachezaji wakati ujao tutajipanga zaidi,” .

Baada ya mchezo huo kiungo mzawa wa Klabu ya Yanga, Fei Toto alionekana akitokwa na machozi ambapo jitihada za kurejesha kwenye hali ya kawaida zilifanywa na Kibwana Shomari, meneja Hafidh Saleh.

SOMA NA HII  YANGA NA PACOME MPAKA AFCON