UONGOZI wa Klabu ya Simba umesema kuwa umejipanga kikamilifu kuhakikisha unafanikiwa kuvuna pointi tatu katika uwanja wa nyumbani dhidi ya Al Ahly.
Simba inatarajia kuvaana na Al Ahly, Februari 23 jijini Dar ikiwa ni mchezo wa pili wa makundi wa Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kumalizana na AS Vita ya DR Congo na ilishinda bao 1-0 nyumbani kwao.
Bao la ushindi lilipachikwa kwa mkwaju wa penalti na mshambuliaji wao Chris Mugalu dakika ya 60.
Katibu wa Simba, Dk Arnold Kashembe amesema kuwa, mipango yao yote juu ya mechi dhidi ya Al Ahly inakwenda kama ilivyopangwa, kila kitu kipo vizuri.
“Maandalizi yetu katika mechi yetu dhidi ya Al Ahly yanakwenda vizuri kama tulivyopanga kuhakikisha tunafanikiwa kushinda hapa nyumbani ambapo ndiyo lengo letu kubwa, kila kitu kinakwenda vizuri, hakuna shida, tunawasubiria wapinzani wetu wakati wowote wanaweza kutua,”.
Simba ipo nafasi ya pili katika kundi lake A la Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa na pointi tatu na bao moja huku Al Ahly inayoongoza ikiwa na pointi 3 na mabao 3 mkononi iliyowafunga Al Merrikh, wanaoshikilia mkia katika kundi lao.
Al Ahly wanatarajiwa kutua usiku wa leo Dar wakitokea Misri kwa ajili ya kukamilisha maandalizi ya mwisho ya mchezo huo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.
Mkurugenzi wa ufundi wa Klabu ya Al Ahly, Sayed Abdelhafiz amesema wanatarajia kuanza safari ya kuja Tanzania kucheza na Simba, Ijumaa na kutua leo Jumamosi lakini amesisitiza wanakuja nchini kwa lengo la kuchukua pointi tatu dhidi ya wapinzani wao.
Akizungumza na mtandao wa timu hiyo, Sayed amesema: “Haikuwa mechi rahisi dhidi ya Al Merrikh lakini tumepata ushindi, tuna furaha juu ya hilo, sasa tunajiandaa na safari ya kuelekea Tanzania siku ya Ijumaa kwa ajili ya mechi yetu dhidi ya Simba.
“Simba ni timu kubwa na wanacheza soka zuri la kuvutia lakini matumaini yetu tutakuwa na mchezo wenye matokeo mazuri ambao utatuwezesha kurejea Cairo na pointi tatu,” amesema Sayed.