Home Simba SC GOMES KATIKA MTIHANI MGUMU SIMBA

GOMES KATIKA MTIHANI MGUMU SIMBA


KWANZA nianze kwa kuwapongeza Simba kwa mafanikio makubwa waliyoyapata kupitia michuano ya Simba Super Cup, ambayo ilianza kutimua vumbi kuanzia Jumatano iliyopita.

Michuano hiyo iliyofikia kilele siku ya Jumapili ilishirikisha timu tatu za TP Mazembe ya Congo, Al Hilal ya Sudani na wenyeji klabu ya soka ya Simba iliandaliwa rasmi kama sehemu ya maandalizi ya timu hizo kujiandaa na michezo ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika.

Naamini michuano hiyo imekuwa na tija kubwa kwa timu shiriki hasa katika kipindi hiki ambacho bado maambukizi ya virusi vya Corona yamekuwa hatari maeneo mbalimbali duniani kiasi cha kusababisha hata baadhi ya ligi kusitishwa.

Kutokana na changamoto hiyo ya ligi nyingi kusimama kwa muda mrefu, wachezaji wanaocheza kwenye ligi husika wamekuwa wakikumbana na tatizo kubwa la kukosa utimamu wa mwili ‘Match Fitness’ hivyo kuhatarisha utendaji kazi wao viwanjani.

Hivyo naamini hili haliwezi kuwa tatizo tena kwa upande wa klabu ya Simba, kwa kuwa wao wamepata muda mwingi wa kucheza kwa kulinganisha na wapinzani waliopangwa nao.

Lakini pia Simba wamenufaika sana na ubora wa timu walizokutana nazo, kwa kuwa walialika timu ambazo zinawiana kwa kiasi kikubwa na zile ambazo wamepangwa nazo katika hatua ya makundi.

Simba ikiwa katika kundi A pamoja na timu za Al Merrikh ya Sudani, AS Vita ya DR Congo na bingwa mtetezi wa michuano hiyo klabu ya Al Ahly kutokea nchini Misri.

Hivyo ni wazi kuwa Simba imepata kipimo na majaribio sahihi ya mitihani ambayo watakwenda kukutana nayo kwenye michezo ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kitu kingine nilichokipenda kutoka Simba hasa katika kampeni yao ya kuhitaji kutinga hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ni usajili walioufanya kwa lengo la kukiongezea nguvu kikosi chao.

Limekuwa jambo la kupongezwa kuona Simba ikitilia maanani na kufuata ushauri wa kocha wao aliyepita, Sven Vandenbroeck ambaye alionya uwezekano wa baadhi ya timu kutumia hujuma ya janga la Corona kudhibiti baadhi ya wachezaji muhimu wa vikosi vya wapinzani.

SOMA NA HII  BAADA YA KUMALIZA USAJILI....MAAMUZI YA BENCHIKHA KWA MASTAA WAPYA SIMBA HAYA HAPA...

Hivyo wamefanya hivyo ili kuhakikisha wanakuwa na kikosi kipana na ndicho ambacho wamekifanya.

Licha ya maandalizi hayo mazuri na ya kupongezwa, kwa upande wangu nadhani Simba bado wana vitu vingi vya kufanya kuelekea michezo hiyo na hawapaswi kubweteka kwa kudhani watakutana na ushindani rahisi.

Kwa kuanzia wakumbuke kuwa ratiba ya michezo hiyo haipo mbali bali ni tarehe 12 tu ya mwezi huu wa Februari, na ikumbukwe bado wana vibarua vya michezo yao ya viporo.

Nadhani wakati huu mtihani ni mkubwa kwa kocha wa Simba Didier Gomes Da Rosa ambaye Wanasimba na wadau wa soka Tanzania wanatamani kuona ni nini atakifanya ili Simba ifuzu hatua ya robo fainali na hatimaye nusu fainali pamoja na kurejea tena kileleni mwa msimamo.

Uchambuzi wa Edibily Lunyamila kupitia gazeti la Championi Jumatatu