Wakati mashabiki na wanachama wa Yanga wakiwa na shauku ya kujua nani atachukua mikoba ya kuinoa timu yao, makamu mwenyekiti wa kamati ya mashindano ya Yanga SC, Mhandisi Hersi Said ameanika hatma ya kocha mpya.
Yanga iko kwenye mchakato wa kutafuta kocha mpya baada ya kuachana na Cedric Kaze hivi karibuni.
“Ijumaa ijayo ndiyo tutamtambulisha rasmi kocha wetu mpya,” amesema Hersi leo wakati akizungumza na Mwananchi Digital.
Amesema walianza kupitia wasifu ‘CV’ wa makocha walioomba kuinoa Yanga tangu Ijumaa iliyopita.
“Tumepokea CV nyingi sana, hivyo zoezi la mapitio bado linaendelea hadi Jumatatu (kesho), kisha tutaingia kwenye hatua ya pili, lakini hadi Ijumaa ijayo tutamtangaza kocha mpya,” amesema.
Alisema hivi sasa wako katika hatua ya mwisho ya kuwachambua makocha wote walioomba ajira ya kuinoa timu hiyo.
“Wapo baadhi ambao tumeshawachuja, ambao wanastahili kuingia kwenye kinyang’anyiro tunawaweka pembeni, wasio na sifa wanatoka,” amesema Hersi ambaye pia ni mkurugenzi wa uwekezaji wa GSM.
Amesema kikao cha mwisho kitakuwa ni kupitia tena majina ya makocha waliopenya katika mchujo wa awali ili kupata mmoja wa kuinoa timu hiyo.
“Tutawasiliana na wale watakaopita kwenye mchujo ili kujua ‘status’ zao, kwani mwingine anaweza kukwambia bado anatimu au anaweza kuja mwisho wa msimu, kuangalia mshahara na yote hayo yatakamilika kabla ya Alhamisi Ijayo na Ijumaa tutamtangaza rasmi kocha mpya,” amesema.