INAELEZWA kuwa Klabu ya Al Ahly ya Misri ipo kwenye hesabu za kuwanasa nyota wawili wa Klabu ya Simba ili kuongeza nguvu kwenye kikosi hicho kinachotetea ubingwa wa Afrika katika Ligi ya Mabingwa inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika, (Caf).
Al Ahly inayonolewa na Pitso Mosimane ipo kundi moja na Simba ambapo kwenye mchezo wao wa kwanza wa kundi A uliochezwa Uwanja wa Mkapa ilikubali kichapo cha bao 1-0.
Mfungaji wa bao hilo, Luis Miquissone anatajwa kuwekwa kwenye rada za mabosi hao wa Afrika huku nyota mwingine anayetajwa kuingia kwenye hesabu zao ni pamoja na kiungo Clatous Chama.
Licha ya kwamba Chama amekuwa akilaumiwa kwamba kasi yake imepungua msimu huu kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika bado amekuwa imara akiwa ndani ya uwanja kwa kuwa alihusika kutoa pasi ya bao ambalo liliwapa pointi Simba mbele ya Al Ahly, Uwanja wa Mkapa.
Habari kutoka ndani ya Simba zimeeleza kuwa ni timu nyingi ambazo kwa sasa zinawafuatilia wachezaji wa timu hiyo hivyo mambo yakiwa sawa kila kitu kitawekwa wazi.
“Unajua kwa namna ambavyo kwa sasa Simba inafanya vizuri kimataifa basi kuna timu nyingi zinawatazama wachezaji wetu, huyu wanamuita Luis, Chama acha tu wewe subiri uone baada ya muda kila kitu kitawekwa wazi,” ilieleza taarifa hiyo.
Hivi karibuni Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara alipokuwa akizungumza na Global Radio, aliweka wazi kuwa wanatambua Luis pamoja na wachezaji wengine watakuwa wanawindwa hivyo bei yao haitakuwa ya kitoto.