Home Simba SC GOMES AWAANDALIA DARASA WACHEZAJI SIMBA NAMNA YA KUIFUNGA AS VITA DAR

GOMES AWAANDALIA DARASA WACHEZAJI SIMBA NAMNA YA KUIFUNGA AS VITA DAR


KOCHA wa Simba, Didier Gomes amewaahidi mashabiki kwamba watapambana ndani ya muda uliobaki kufanya mambo mazuri haswa kimataifa.

Gomes alisema anategemea kuwa na kikosi chake chote kambini Aprili 1 na wataikabili mechi hiyo ya AS Vita kisayansi zaidi haswa wakikumbuka sare ya mabao 2-2 ya Vita na Ahly kule Misri.

Alisema kutokana na pointi zao kumi ambazo wanazo wakati huu ili wawe na uhakika wa kwenda hatua inayofuata lazima washinde dhidi ya Vita na kama ikishindikana wapate sare.

“Kutokana muda ni mchache wa kuwa pamoja na kikosi changu kamili nimeamua kuandaa darasa ambalo na wachezaji wangu wote pamoja na wasaidizi wangu,” alisema Gomes akiizungumzia mechi hiyo ya Jumamosi Kuu ya Pasaka.

“Katika hilo darasa tutakuwa tukiangalia video mbalimbali za mechi ambazo AS Vita wamecheza katika hatua ya makundi ikiwemo ile ya kwetu ambayo tuliwafunga pamoja na michezo yao ya ligi,” alisema Kocha huyo ambaye ameimudu morali ya wachezaji wa Simba.

“Binafsi nimeshafanya hilo na kuna vitu ambavyo nimegundua ila sasa nataka kuwaonyesha wachezaji wangu nao waelewe mambo ya kwenda kufanya katika dakika 90 za mchezo.

“Baada ya kuangalia hizo video Aprili 2(Ijumaa Kuu), tutafanya mazoezi mepesi ya uwanjani kwa vitendo vile ambavyo tuliviona kupitia video kutoka kwa AS Vita jinsi ya kuwazuia na kuwashambulia,” alisema Gomes ambaye ni kocha wa zamani wa El Merrikh ya Sudan.

“Kutokana na plani hiyo ya maandalizi ambayo tumeiweka maana yake mbinu au mchezo ambao tulicheza nao katika mechi ya kwanza licha ya kuwafunga itakuwa tofauti na huu ambao tutacheza hapa nyumbani kwani tumepanga kufanya mashambulizi mengi na kutengeneza nafasi za kufunga ili kumaliza mechi mapema.”

Katika hatua nyingine licha ya ugumu wa ratiba ya Shirikisho la soka Afrika (CAF), bahati nzuri kwao wachezaji wake wengi wapo katika kikosi cha Taifa Stars ambao mechi ya mwisho wanacheza Machi 28, hapa Dar es Salaam na haraka watajiunga na kambi.

SOMA NA HII  EDO KUMWEMBE - PAMOJA NA KUWA ANA 'HOMA YA VIPINDI'..GOLI LA MORRISON LITAIBEBA SIMBA CAF...

Gomes alisema mechi na AS Vita kama imeshika hatma yao ya kucheza robo fainali itakuwa ngumu kwani wapinzani wao hawatakubali kufungwa mara mbili na wao wanatafuta pointi ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kusonga hatua ijayo.

“Kama tungepata muda wa kutosha maana yake tungeweza kuweka mipango yetu mingi sawa tukiwa kwa pamoja lakini haina jinsi kutokana na mazingira yalivyo tutaandaa timu ili kwenda kuvuna pointi tatu katika mechi hiyo,” alisema Gomes na kuwataka mashabiki wasiwe na wasiwasi hata kama hawataingia uwanjani.

Simba inaongoza kundi A la Ligi ya Mabingwa Afrika.