KOCHA Mkuu wa Yanga, Juma Mwambusi, amesema kuwa kama atawapata wachezaji wake wote waliokwenda kuzitumikia timu zao za taifa wakiwa salama akiwemo staa Saido Ntibazonkiza na Mukoko Tonombe basi anaamini wataisaidia timu hiyo katika michezo yao inayofuata ya ligi.
Wachezaji wa Yanga ambao walikwenda kuzitumikia timu zao za taifa ni pamoja na Saido Ntibazonkiza (Burundi), Tonombe Mukoko (Congo) na Haruna Niyonzima (Rwanda), Feisal Salum, Bakari Mwamnyeto na Deus Kaseke wote kutoka Tanzania.
Mwambusi amesema kuwa, hali ya kikosi chake kilichopo kambini ipo sawa kwa wachezaji waliosalia kambini huku akisema kuwa ana matumaini na wachezaji walioenda kuzitumikia timu za taifa wakiwemo Saido, Mukoko Tonombe.
Anaamini kuwa ikiwa watarejea wakiwa wataisadia Yanga katika michezo inayofuata ya Kombe la Shirikisho na ligi kuu.
“Hali ya wachezaji wetu kambini ni nzuri, wachezaji wanaonyesha kufurahia mazoezi, wanajituma tayari kwa ajili ya maandalizi ya michezo yetu ijayo ya Kombe la Shirikisho na ligi kuu.
“Kwa wale wachezaji ambao walienda kuyatumikia mataifa yao, kiu yetu ni kuona kuwa wanarejea wakiwa salama kwani watatusaidia sana katika michezo yetu ijayo, unafahamu kuna kipindi timu ilikuwa na majeraha kwa wachezaji muhimu hivyo hatutamani kuona likitokea tena,” alisema kocha Mwambusi.