UONGOZI wa Klabu ya Yanga, umerejea kwa kasi kwenye mchakato wa kuchambua jina moja la mrithi wa Cedric Kaze aliyetimuliwa Machi 7, mwaka huu.
Mchakato huo ulisimama kwa muda wa siku 21, kupisha maombolezo ya kifo cha Hayati, Dk John Pombe Magufuli, ambapo majina ya kocha wa zamani wa timu ya Township Rollers ya Botswana, Nikola Kovazovic, aliyekuwa Kocha wa TP Mazembe ya DR Congo, Hubert Velud na kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Kenya, Mfaransa, Sebastian Migne ndiyo yanatajwa kuwa na nafasi kubwa ya kubeba mikoba hiyo.
Kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele, Yanga wamekuwa wakigubikwa na hali ya kukosa utayari wa chaguo sahihi, ambapo tangu wamuondoe Kaze kwa madai ya kutoridhishwa na matokeo, sasa wamerejea upya kwenye mchakato huo, ili waweze kupata jina mojawapo mapema kabla ya mechi yao ya marudiano na Simba ya Mei 8, mwaka huu kufika.
Chanzo makini kimeliambia Championi kuwa, tayari Kamati ya Utendaji ya Yanga, imeingia tena kwenye mchakato huo, ili uweze kujihakikishia jina moja la kocha ambaye anatakiwa kuwa ndani ya nchi muda wowote kuanzia sasa ili aweze kuja kuzoea mazingira na kuona mechi yao dhidi ya Simba.
“Hatimaye sasa furaha inaenda kurejea ndani ya klabu yetu, ambapo tayari uongozi wetu kupitia kamati ya utendaji na wadhamini wetu, GSM wameanza upya kujielekeza kwenye suala la kocha, ambapo, wana mpango wa kuitisha kikao cha dharula ili kuhakikisha kocha anatua kabla ya mechi yetu na Simba,” kilisema chanzo hicho.
Kwa upande wa Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli alisema: “Ishu ya kocha tayari tumeshaiweka wazi kuwa majina matatu yapo na kweli siku chache zijazo kamati tendaji itakaa na kupendekeza jina la kocha mmojawapo ambaye muda wowote ataungana nasi.”