NYOTA wa Yanga, Saido Ntibanzokiza amesema kuwa hana tatizo lolote na wachezaji wake pamoja na benchi la ufundi bali ni sehemu ya mchezo ambayo ilitokea jana wakati timu hiyo ikishinda mabao 3-1 dhidi ya Gwambina FC.
Katika mchezo wa jana uliongozwa na Kaimu Kocha, Juma Mwambusi, Saido alianzia benchi na aliingia kipindi cha pili akichukua nafasi ya Tuisila Kisinda ambaye aliumia alipofunga bao hilo hakushangilia.
Hali hiyo ilionyesha kuwa nyota huyo hakuwa na furaha kuanzia benchi pia hakukuwa na mawasiliano mazuri na kiungo Deus Kaseke baada ya kuingia ndani ya uwanja.
Aliweza kupachika bao la tatu kwa Yanga dakika ya 90+4 akitumia pasi ya Michael Sarpong na baada ya kufunga bao hilo alianza kuonyesha ishara kwamba atolewe nje jambo ambalo alilifanya ghafla huku akionekana kuvua jezi ya Yanga.
Akizungumzia suala hilo kiungo huyo raia wa Burundi amesema:”Ni mechi ambayo tulikuwa tunahitaji ushindi na tumepata hilo tunamshukuru Mungu.
“Wachezaji tupo vizuri isipokuwa muda mwingine huwa inatokea kwenye mchezo na pale mchezo unapokwisha hayo yanakuwa yanaisha. Kikubwa ni ushindi na hiyo ndiyo furaha yetu,”.
Yanga inafikisha jumla ya pointi 57 ikiwa nafasi ya kwanza baada ya kucheza jumla ya mechi 26 Gwambina wanabaki nafasi ya 12 na pointi zao ni 30.