ZIKIWA zimesalia siku mbili kabla ya kufikia siku ya mchezo wa watani wa jadi, Simba na Yanga, beki wa kati wa zamani wa timu hizo, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’, amesema kuwa licha ya Simba kufanya vizuri na kuwa na kikosi kizuri lakini wanatakiwa wasiwadharau Yanga kwani wanayo nafasi ya kufanya vizuri katika mchezo huo.
Bakari Malima baada ya kustaafu kucheza soka kwa sasa amegeukia kazi ya ukocha wa mpira, enzi zake alipokuwa mchezaji aliwahi kuzichezea timu hizo zote mbili za Simba na Yanga katika vipindi tofauti.
Malima amesema kuwa licha ya ubora walionao Simba, wanatakiwa wasiwadharau wapinzani wao kwani wana uwezo mkubwa wa kupata matokeo mbele yao huku akiwasisitizia Yanga kujipanga vizuri ili waweze kupata matokeo mbele ya Simba.
“Simba wanayo timu nzuri ya kupambana, wanao wachezaji wengi wakubwa na wenye uzoefu lakini hiyo sio sababu ya kusema kuwa tayari wameshaibuka na ushindi dhidi ya Yanga, kwani wakiwachukulia poa, wanaweza kujikuta wamefungwa na Yanga.
“Kwa upande wa Yanga wanatakiwa kutohofia mchezo huu kwani hakuna dabi nyepesi siku zote, hata sisi wakati tunacheza ulikuwa msimu wa 1994/95 tuliwahi kukutana na mechi ambayo Simba walikuwa na majina makubwa na fomu nzuri lakini tulipambana na tukapata matokeo, hivyo hata sasa hivi Yanga wakipambana wanaweza kuwafunga Simba,” amesema Malima.
Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa, Mei 8, ule wa kwanza uliochezwa Novemba 7, ubao ulisoma Yanga 1-1 Simba.
Chanzo:Championi