UONGOZI wa Simba umeibuka na kufungukia sakata la wao kufungiwa kufanya usajili kwa kipindi cha msimu mmoja na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).
Taarifa hizo za kufungiwa Simba zilienea hivi karibuni kwa kile kilichotajwa kushindwa fidia za kuvunja mkataba wa aliyekuwa beki wao wa pembeni, Mghana Asante Kwasi.
Katika taarifa hiyo ilielezwa Simba imefungiwa baada ya kushindwa kumlipa fidia ya Sh 9Mil baada ya kuvunja mkataba wa kuendelea kuichezea timu hiyo.
Mkuu wa Kitengo cha Mahudhui cha Simba, Ally Shatry alisema kuwa hizo taarifa hazina ukweli wowote za wao kufungiwa huku akiwataka mashabiki wa timu hiyo kuachana nazo.
Shatry alisema kuwa, hizo ni proganda zilianzishwa kwenye mitandao ya kijamii zenye lengo la kuwaondoa kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara.Aliongeza kuwa hakuna barua yoyote ya kiofisi waliyopokea kutoka Fifa kuhusiana na taarifa hizo, kama zingekuwa za kweli basi wangeandikiwa barua na shirikisho hilo.
“Kinachoendelea sisi tunakijua kila kitu, hizo ni propaganda zenye lengo baya za kutuchafua na kututoa kwenye mbio zetu za ubingwa wa ligi.
“Katika kuthibitisha hilo hakuna barua yoyote tuliyopokea kutokea Fifa hata hilo shirikisho hilo halifanyi kazi na mitandao ya kijamii iliyovumisha taarifa hizo.
“Kama uongozi tumezipuuza taarifa hizo na badala yake nguvu na akili zetu tunazielekeza katika mchezo ujao wa ligi ,” alisema Shatry.
Alipotafutwa Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’, Cliford Ndimbo kuhusiana na ishu hiyo alisema: “Mpaka sasa kwenye idara yangu ya habari taarifa hiyo haijafika, nami ninaiona kwenye mitandao, ninasubiri ikifika tutatoa taarifa rasmi juu ya ishu hiyo.”
Chanzo:Championi