KAMA unadhani baada ya kuahirishwa kwa mchezo kati ya Simba na Yanga kuliwaumiza mashabiki pekee, basi sahau hilo kwani hata upande wa wapinzani wa Simba kimataifa timu ya Kaizer Chief imeumia pia.
Ikumbukwe kuwa Simba katika mchezo wa hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika wamepangwa kucheza na timu hiyo ya nchini Afrika Kusini, mechi ikitarajiwa kuchezwa Jumamosi hii nchini Afrika Kusini kabla ya kurudiana wiki ijayo.
Chanzo cha ndani cha Simba, kililithibitishia Championi Jumatatu kuwa, Kaizer Chiefs walituma mashushushu wao kuja kuichunguza Simba ikicheza dhidi ya Yanga jambo ambalo lilikwama kutokana na mchezo huo kuahirishwa.
“Katika mchezo wetu ambao ulitakiwa ufanyike dhidi ya Yanga, tayari kulikuwa na wawakilishi wa Kaizer Chiefs, yaani maskauti wao ambao walikuja kuichunguza au kuitazama Simba ikicheza dhidi ya Yanga.
“Lakini kwa bahati mbaya mchezo huo haukufanyika, hivyo dhamira yao haikutimia, walikuja watatu ambao walitua hapa nchini Ijumaa iliyopita, siku moja kabla ya mchezo,” kilisema chanzo hicho.
Simba inatarajiwa kucheza na Kaizer Chiefs Jumamosi hii katika Uwanja wa Soccer City nchini Afrika Kusini katika mchezo wa robo fainali ya kwanza.