LICHA ya kwamba mabosi wa Simba wanalalamika kutocheza na Yanga kwenye mechi ya Dabi ya Kariakoo, Mei 8 lakini uchunguzi wa Championi Jumatano, unaonyesha wazi wao ndiyo wamefaidika kwa kiwango kikubwa kuliko watani zao.
Faida hiyo ambayo wameipata Simba ni wakati huu ambao wanajiandaa kucheza na Kaizer Chiefs katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya robo fainali.
Dabi hiyo ya Simba na Yanga iliahirishwa kutokana na mabadiliko ya muda wa awali ambao ulikuwa ni saa 11:00, kisha kusogezwa mbele hadi saa 1:00 usiku na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
TFF ilieleza kuwa imetoa taarifa kwa timu zote mbili kuhusu mabadiliko ya muda huo kupitia kwa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB).
Yanga walienda uwanjani saa tisa kwa ajili ya mchezo wa saa 11 na Simba wakaenda saa 11 kwa ajili ya mchezo wa saa 1 kamili.
Taarifa iliyotolewa kwa sasa na TFF ni kwamba mchezo huo utapangiwa tarehe pamoja na muda baada ya pande zote kukaa kikao.
Faida ambazo Simba wamenufaika nazo kutokana na kuota mbawa kwa dabi hiyo wakati huu wakicheza na Kaizer Chiefs ni kama ifuatavyo:
MAJERAHA
Kutocheza mchezo huo kumefanya asilimia kubwa ya wachezaji wa kikosi cha Simba kuwa salama kwa kuwa rekodi zimekuwa zikionyesha kuwa Kariakoo Dabi huwa inaleta wachezaji majeruhi kutokana na matumizi ya nguvu kubwa.
Simba Januari 4, 2020, kwenye mchezo wao dhidi ya Yanga uliokamilika kwa sare ya kufungana mabao 2-2, Deo Kanda, Mzamiru Yassin na Meddie Kagere walipata majeraha ambayo yaliwafanya wakae nje kwa muda.Pia Machi 8, wakati ubao wa Uwanja wa Mkapa ukisoma Simba 0-1 Yanga, kiraka Erasto Nyoni alipata majeraha ambayo yalimuweka nje kwa muda mrefu.
FATIKI
Kutokana na matumizi mengi ya nguvu katika mechi ya watani wa jadi ambayo Simba wangeitumia ni dhahiri kwamba wangekuwa na kile kinachoitwa fatiki (uchovu), kinachotokana na matumizi makubwa ya nguvu.Kutochezwa kwa mchezo huo ni fursa kwa wachezaji kuwa katika hali ile ya kawaida na kuingia uwanjani wakiwa na nguvu mpya.
WAMEWAPIGA CHENGA KAIZER CHIEFS
Ipo wazi kwamba mashushushu kutoka Afrika Kusini walikuja Bongo ili kushuhudia mchezo huo na kuiba mbinu za Gomez. Kutokana na ukubwa wa mechi hakuwa na ujanja wa kuficha wachezaji wake muhimu kwa namna yoyote ile, ilikuwa ni lazima kuachia kikosi kazi.
Ndivyo ilivyokuwa hata baada ya Simba kuachia kikosi ambacho kilitarajiwa kucheza mchezo huo kilikuwa ni kile ambacho huwa kinaanza kwenye mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika.Hivyo mchezo huo kutochezwa imekuwa ni salama ya Simba kupata faida ya mbinu zao kutoibiwa na wapinzani.
HASIRA ZOTE KWA KAIZER CHIEFS
Hasira za wachezaji za kushindwa kupata matokeo kwenye mchezo wa kwanza Novemba 7, ubao uliposoma Yanga 1-1 Simba, zilikuwa zimekusanywa na wachezaji na benchi ili kuzimaliza Mei 8. Kuyeyuka kwa mchezo huo kunawafanya Simba kusepa na hasira zao kuzipeleka kwa Wasauzi hao, Kaizer Chiefs.
MORALI KUBWA
Morali mpya na kubwa kwa wachezaji wa Simba itaongezeka kwa sababu hawana presha ya kupoteza mchezo wao wa watani wa jadi. Kama mchezo huo ungechezwa na Simba kufungwa, ile morali ya wachezaji huenda ingepungua na kukosa nguvu ya kufanya vizuri mchezo wao ujao ambao ni wa kimataifa.
KAULI YA SIMBA
Kocha msaidizi wa Simba, Seleman Matola, aliliambia Championi Jumatano kuwa hakuna kilichoharibika baada ya mchezo huo kuahirishwa zaidi wanapiga hesabu mechi zao zijazo.
“Imetokea huwezi kufanya jambo lingine, kuanzia saikolojia na akili za wachezaji zipo sawa kwa ajili ya kutimiza majukumu yao. Imani yetu ni kwamba tunakwenda kucheza na wapinzani wakubwa na wagumu hivyo ni lazima tupambane ili kufikia malengo yetu, suala la Yanga kwenye hili halijabadili mipango.