KIKOSI cha Simba kinachonolewa na Kocha Mkuu, Didier Gomes pamoja na Seleman Matola ambaye ni msaidizi, leo kinatarajiwa kuanza mazoezi ya maandalizi kwa ajili ya mchezo wa marudio dhidi ya Kaizer Chiefs wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kwa mujibu wa Mratibu wa Simba, Abass Ally amesema kuwa wana mlima mzito kwa sasa baada ya kupoteza mchezo wa kwanza kwa ubao wa FNB Soccer City kusoma Kaizer Chiefs 4-0 Simba.
Licha ya kupoteza kwa kufungwa mabao hayo bado wana matumaini ya kufanya vizuri kwenye mchezo wao wa marudio unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa, Mei 22.
“Tuna mlima mzito wa kupanda hasa ukizingatia kwamba mchezo wa kwanza tumepoteza kwa kufungwa mabao manne ila kwenye mpira kila kitu kinawezekana.
“Kwa sasa tupo Tanzania, tunashukuru dua za mashabiki pamoja na sapoti yao kubwa wasikate tamaa, tunaanza maandalizi kwa ajili ya mchezo wetu ujao na kwa uwezo wa Mungu tunaamini tutapata matokeo,” .
Ili iweze kusonga mbele hatua ya nusu fainali ina mlima wa kushinda mabao matano bila kuruhusu nyavu zao kutikiswa mbele ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.