Chini ya Kocha Mkuu, Nassredine Nabi Yanga waliendeleza mwendo wa ushindi baada ya kutoka kushinda mabao 2-0 dhidi ya JKT Tanzania kwenye mchezo wa ligi na jana ilikuwa ni Kombe la Shirikisho hatua ya robo fainali.
Ushindi huo utaifanya timu hiyo kukutana na Biashara United ambayo ilishinda nayo mabao 2-0 dhidi ya Namungo FC katika mchezo wao wa hatua ya robo fainali.
Kaseke alianza kupachika bao la kwanza dakika ya 24 baada ya kipa namba moja wa Mwadui FC, Mussa Mbissa kufanya makosa akiwa na mpira ndani ya 18 ambao aliupoka kwa beki wake yeye mwenyewe.
Kasi ilizidi kipindi cha kwanza ila Mwadui walikuwa imara na kuweza kwenda mapumziko ubao wa Uwanja wa Kambarage ukisoma Mwadui 0-1 Yanga.
Kipindi cha pili, Yanga walianza kwa kasi sawa na Mwadui na ni Yacouba Songne alimtengeneza pasi kiraka Kaseke ambaye hakuwa na ajizi alipachika bao la pili dakika ya 56.
Ingekuwa umakini wa Yanga wangefunga mabao mengi ila shukrani kwa kipa Mbissa ambaye dakika ya 54 aliokoa jaribio la Ditram Nchimbi, dakika ya 53 na 43 aliokoa hatari ya Yacouba na wote walifanya majaribio hayo ndani ya eneo la 18. Nje ya 18 lilikuwa ni jaribio la Kibwana Shomari.
Kaseke naye alikuwa na nafasi ya kufunga mapema dakika ya 10 ila mikono ya Mbissa iliokoa hatari hiyo na licha ya mpira kukutana na Yacouba naye alikosa kupachika bao hilo.
Ni Denis Richard alifanya jaribio moja dakika ya 49 kwa Farouk Shikalo ila liliokolewa , Wallace Kiango alifanya jaribio dakika ya 44, Salim Aziz dakika ya 64 akiwa nje ya 18 alifanya jaribio liliokolewa na Shikalo na kuwafanya washindwe kupata bao na kuaga mashindano hayo.