Home Yanga SC YANGA, PIGA CHINI HAWA

YANGA, PIGA CHINI HAWA


 Na Saleh Ally

INAWEZEKANA nikawa sikufurahishi kutokana na kuwataja wachezaji vipenzi vyako na ushauri wangu ukawa ni kuona wanaachwa, sitajali. Lakini soma kidogo kwa kuwa hawa, naona wanachukua fedha za bure Yanga.


Yanga inapaswa kupata huduma kutokana na kile ambacho inakilipia kwa maana ya kutoa huduma ya mishahara mizuri na huduma nyingine kwa wachezaji wake na hasa wale wa kigeni, sasa wanafanya nini?

 Tujiulize wanaipa Yanga kinachostahili? Binafsi naona hapana lakini naiona hapana hii ingeweza kuwa na nafuu kama ungeona wachezaji hawa wana majuto, wanaonyesha kusikitishwa kulingana na kile wanachoifanyia Yanga lakini imekuwa tofauti.


Baadhi ya wachezaji wamekuwa wakionyesha ujeuri

wa wazi, wamekuwa wakiamini wao ni wakubwa ikiwezekana hata kuliko Yanga yenyewe na huenda wanaamini Yanga haiwezi kwenda bila ya wao.


Kuna mambo matatu makubwa, moja kiwango duni, pili majeruhi na tatu nidhamu mbovu ambayo inaipa Yanga kila sababu ya kuachana na rundo la wachezaji wake wa kimataifa.


Ukiangalia, sote hata Yanga wenyewe hawawezi kukataa ubora wa kiwango cha watani wao, Simba.

Ukiangalia mchango mkubwa wa kiwango bora cha Simba, bila ya ubishi unatengenezwa na wachezaji wa kigeni. Wachezaji wa kigeni wa Yanga mchango wao ukoje?



Mechi zikiwa zimebaki tano kufunga msimu huku Yanga wakiwa wanaufukuzia ubingwa kwa asilimia 35 na zilizobaki ni nafasi ya pili, unaona takribani nusu ya wachezaji wake wa kigeni wako nje ya uwanja wakiwa na matatizo kadhaa, mfano utovu wa nidhamu, majeruhi, kiwango duni au matatizo ya kifamilia.


Wachezaji walio nje bado hawaonyeshi kama kweli wana majeruhi, kwa hali ilivyo bila ya ubishi, baadhi yao inaonekana wamesusa katika kipindi hiki kigumu ambacho Yanga inawahitaji kupambana kwa ajili ya ubingwa na wakiukosa basi kujihakikishia nafasi hiyo ya pili.


Angalia, Azam FC sasa wanaifuata Yanga kwa mwendo wa kutisha kidogo na wamekuwa na mwenendo mzuri. Jambo ambalo Yanga inahitaji kikosi kipana ili kupambana na kuhakikisha wanamaliza katika sehemu hizo mbili za juu.


Hakuna ubishi kama Yanga watazubaa kidogo wanaweza kuingia kwenye mshituko wa kujikuta katika nafasi ya tatu. Lakini angalia wachezaji wa kigeni na wale wa kutegemewa karibu asilimia 60, wako nje ya uwanja kwa sababu ambazo nyingi ni vijisababu.

SOMA NA HII  KAMPUNI 10 ZA KIMATAIFA ZAJITOKEZA KUUJENGA UWANJA WA YANGA KIGAMBONI

Carlinhos ni mmoja wa wachezaji wazuri lakini hata mara moja hajawahi kuichezea Yanga zaidi ya mechi tano mfululizo. Mchezaji wa on, off na kweli akicheza mchango utauona lakini anacheza mechi ngapi angalau mfululizo. 

Angalia wachezaji wa Simba, nani na yupi unaweza kumkosa kila mara kama ilivyo kwa Carlinhos. Kwa uzuri tu Yanga wamuonyeshe njia aende zake.


Sijajua mikataba yao wameipanga vipi na kama kulikuwa na tahadhari, lakini mshambuliaji Michael Sarpong naye hana faida, mabao manne hadi leo na zaidi ya hapo ni mbwembwe tu, hakuna kingine kilichofanyika. Yanga wanapaswa kumuonyesha mlango mapema sana kwa kuwa ni hasara kuendelea kubaki naye, wa nini sasa?


Hawa veteran wawili wa Kirundi, Saido Ntibazonkiza na Abdulazak Fiston nao hawana mchango ambao Yanga wanaweza kujivunia na ukweli ni kwamba wanatumia muda mwingi wakiwa nje ya uwanja.


Mchango wao ni mdogo na mbwembwe ni nyingi, sema mashabiki wa Yanga wanataka furaha, anayewapa kidogo wanaichukulia kama nafuu kubwa lakini kiuhalisia, bado Ntibazonkiza na Fiston hawajafanya kitu kikubwa ambacho Yanga wanaweza wakajivunia sana.


Umeona Fiston akiwa kwenye insta Live akichati na mashabiki wakati Yanga ikipambana uwanjani. Unaweza kusema angeweza hata kutumia muda mwingi kuangalia mchezo na kujua wenzake wanafanya nini. Ntibazonkiza mara ya mwisho kufunga ni lile bao alipoingia akiwa na hasira baada ya Kocha Juma Mwambusi kumuacha nje, akafunga na kuomba atolewe.


Lakini tangu alipoanza kupewa nafasi ya kuanza, hajafunga. Ukweli kwa maana ya hadhi ya wachezaji wa kulipwa wanaofanya kazi yao Yanga vizuri, hakuna kitu na wanastahili kupigwa chini.


Lamine Moro sote tumeona, inawezekana kuna jambo la kusuluhisha kati yake na Yanga na kama limeshindikana, basi naye apigwe chini. Yanga inahitaji watu watakaoipa msaada hasa kwa maana ya kuilipa kutokana na kile inachowalipa.


Niwakumbushe, kama wageni wanalipwa zaidi basi nao wanastahili kutenda na kufanya vizuri zaidi. La sivyo, wakubali kufanya kazi kwa kiwango cha chini.


Mshahara wa Sarpong ukijumlisha na utovu wa nidhamu ni hasara tu kwa Yanga na lazima uongozi Yanga ubungue bongo kwamba kinachoendelea ni kuendelea kujiumiza lakini anayeumia hataki kupiga kelele kwa sauti ya juu kwa hofu ya kuona majirani watamsikia, hivyo amebaki kugugumia tu maumivu.