Home Simba SC USHINDI DHIDI YA YANGA UTATUPA KUJIAMINI ZAIDI – GOMES

USHINDI DHIDI YA YANGA UTATUPA KUJIAMINI ZAIDI – GOMES

 


KOCHA wa Simba, Didier Gomes amesema mechi yao na Yanga ndiyo itakayomuongezea kujiamini zaidi kuelekea mchezo wa robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Kaizer Chiefs itakayochezwa nchini Afrika Kusini.

Gomes ambaye ni Mfaransa, amesema anaandaa mipango kamilifu ya kimbinu kuhakikisha wanawazidi Yanga na kuwafunga ili morali kwa wachezaji wake iwe juu wakati wanakutana na Kaizer.

“Kama tukiwafunga Yanga ni wazi tutakwenda kukutana na Kaizer tukiwa vizuri ndio maana tumedhamiria kulifanya hilo, na kutokana na wachezaji wangu walivyo inawezekana,” alisema Gomes na kuongezea;

“Nimetenga muda wa kutosha na wasaidizi wangu kuona mambo mengi kutoka kwa Yanga, kuna maeneo wapo bora na palipokuwa na udhaifu kote tumefanyia kazi tukiwa na wachezaji wote.

Katika hatua nyingine, Gomes alisema katika kuhakikisha anapata ushindi kwenye mchezo huo amebadilisha ratiba kwa wachezaji wake.

Alisema baada ya kuingia kambini jana Jumatatu wachezaji wake wa kikosi cha kwanza walifanya mazoezi mepesi na laini ili kuweka miili yao sawa wakati wale wengine watakuwa wanaendelea na ratiba ya kawaida.

Alisema leo Jumanne wachezaji hao wa kikosi cha kwanza watakuwa na ratiba ya kufanya mazoezi ya Gym, kuingia katika maji yaliyochanganywa na barafu pamoja na mengine laini ili kuweka misuli yao sawa.

“Baada ya hapo siku zilizobaki nitawaunganisha kwa pamoja uwanjani ili kufanya kwa vitendo yale ambayo tuliyaona kwa wapinzani wetu na awali tulikuwa tukielekezana kwa maneno,” alisema.

Kuhusu kiwango cha Morrison, kocha huyo alisema kuwa; “Ni mchezaji mzuri, maalumu, mwenye kipaji kikubwa lakini huwa si mzuri katika kukaba lakini kwenye mchezo huo atakuwa ndani ya orodha ya wachezaji 18 ila ataanzia benchi na kuingia kipindi cha pili.

“Yote hayo tunayafanya ili kupata ushindi wa kutosha dhidi ya Yanga ingawa nafahamu utakuwa mchezo mgumu kutokana nao wanahitaji zaidi pointi dhidi yetu.”

SOMA NA HII  SIMBA MDOMONI MWA VINARA CAF...PABLO AINGIA UBARIDI...KOCHA WA ASEC AIPA UBINGWA SIMBA...