Home Yanga SC YANGA YATAMBA HAINA HOFU KWENYE KOMBE LA FA, WANAHITAJI UBINGWA

YANGA YATAMBA HAINA HOFU KWENYE KOMBE LA FA, WANAHITAJI UBINGWA


 BAADA ya kuifungashia virago Tanzania Prisons na kutinga hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam maarufu Kombe la FA, uongozi wa Klabu ya Yanga umesema kuwa hawaihofii timu yoyote watakayocheza nayo, hivyo wako tayari.

 

Yanga wametinga hatua hiyo baada kuwafunga Prisons bao 1-0 katika mchezo mkali wa hatua ya 16 bora uliopigwa kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, Sumbawanga mkoani Rukwa.

 

 Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Haji Mfikirwa, amesema: “Kwanza kabisa tunashukuru kwa kufikia hatua hii ya robo fainali, huu ni mwendelezo wa malengo ambayo tumejiwekea msimu huu.


“Tayari tumechukua Kombe la Mapinduzi na sasa tunapambana kuhakikisha tunatinga fainali na kutwaa kombe hili la FA.

 

“Tunajua wazi haitakuwa kazi rahisi kutokana na ugumu wa michuano hii, kwani kila mmoja ameona mchezo wetu ulivyokuwa mgumu, lakini niwahakikishie kuwa tumejipanga vizuri na hatuihofii timu yoyote tutakayopangwa nayo. Tumejipanga kucheza kila mchezo kama fainali ili kutimiza lengo letu.

 

“Katika kuongeza motisha juu ya hilo, uongozi umejipanga vizuri kuongeza hamasa ndani ya kikosi chetu katika namna mbalimbali ikiwemo bonasi za wachezaji kuelekea hatua zinazofuata,” .


Miongoni mwa timu ambazo zimetinga hatua ya robo fainali ni pamoja na Rhino Rangers inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza, Dodoma Jiji, Simba ambao ni mabingwa watetezi, Namungo, Azam FC, Mwadui FC.


SOMA NA HII  KUELEKEA MECHI ZA CAF...EDO KUMWEMBE AWAPASULIA UKWELI HUU YANGA...