SIMBA imepata majina ya Wazambia wawili ambao inawaandaa kuwa mbadala wa Luis Jose ambaye dili lake la kuuzwa pesa nyingi liko kwenye mstari.
Kuna mipango inaendelea kimyakimya ndani ya Simba na kama timu mbili za Morocco na Misri zitafika dau la Sh 2Bilioni na ushee, Wekundu hao watamuuza Luis kiroho safi.
Wazambia wawili washambuliaji, Moses Phiri anayecheza Zanaco ya Zambia pamoja na Justin Shonga anayekipiga Cape Town FC ya Afrika Kusini ndio mmoja wao anapewa nafasi kubwa ya kuchukua nafasi ya Luis, lakini dili likikwama wataangalia njia mbadala.
“Kuhusu Phiri na Shonga majina yao tunayajadili, ila wengi wanaonekana kuwakubali na ila tunachoangalia sasa ni idadi ya wachezaji wa kigeni 10 ambao wapo katika kikosi chetu, kilisema chanzo chetu na kuongeza;
“Ambacho kipo ni kwamba huenda tukamtoa kwa mkopo, Perfect Chikwende na nafasi yake akaingia kiungo mmoja kati ambaye kocha anamfuatilia au mmoja kati ya Phiri na Shonga.”
“Ili kukamilisha dili la Phiri au Shonga tunasubiri kama Luis tunaweza kumuuza kwa dili la maana ambalo halitakuwa chini ya Dola za Kimarekani 700,000 (Zaidi ya Sh2Bilioni) mpaka Dola 1 milioni na mshahara mzuri tunaweza kumuachia akatafute changamoto mpya na nafasi yake ndio inaweza kuzibwa na nyota hao wawili,” alidokeza kiongozi huyo huku akisisitiza hawawezi kumuuza Luis kwa pesa ya kawaida kutokana na ubora na umri wake.
Licha ya kutotaja timu zinazomuwania Luis, lakini alisisitiza kwamba kuna dili kadhaa zuri ziko mezani wanaendelea kuelewana na hizo timu kama mambo yakikaa kwenye mstari watamuachia staa huyo na kuvuta mmoja kati ya Shonga na Phiri ambao wote ni moto na Kocha Didier Gomes anawajua.
Taarifa nyingine kutoka Afrika Kusini zinasema kuwa Shonga huenda akaachana na Cape Town kwa kulazimisha kuvunja mkataba wake kwa sababu ya kutokuwa kipenzi cha kocha wa timu hiyo.
Wachambuzi kadhaa wamekuwa wakiwasihi Simba kusajili kiungo mwenye uwezo wa kucheza namba nane badala ya kuwatumia zaidi Thadeo Lwanga, Mzamiru Yassin, Erasto Nyoni na Jonas Mkude ambao wote kiasili ni wakabaji si washambuliaji.
Simba imepanga kufanya usajili makini kuimarisha kikosi chao ambacho kimeishia kwenye hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.