MENEJA wa timu ya taifa ya Tanzania, Nadir Haroub, ‘Canavaro’ amewaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi Uwanja wa Mkapa kushuhudia mchezo wa kirafiki dhidi ya timu ya taifa ya Malawi.
Stars inayonolewa na Kocha Mkuu, Kim Poulsen iliingia kambini Juni 5 kwa ajili ya maandalizi ya mchezo huo uliopo kwenye kalenda ya Fifa unaotarajiwa kuchezwa leo Juni 13, Uwanja wa Mkapa.
Miongoni wa wachezaji ambao walianza mazoezi ni pamoja na Dickson Job, Bakari Mwamnyeto, Shomari Kapombe, John Bocco, Idd Suleman, Salum Aboubakary, Edward Manyama.
Akizungumza na Saleh Jembe, Canavaro amesema kuwa ni muhimu kwa mashabiki kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu yao kwa kuwa mashabiki ni muhimu kwao kuipa sapoti timu yao.
“Hii ni timu ya kila Mtanzania hivyo itapendeza ikiwa watajitokeza kwa wingi kutoa sapoti kwa wachezaji ambao wanawakilisha taifa letu. Imani yangu kila mmoja anapenda kuona wachezaji wakicheza basi wajitokeze kwa wingi.
“Mpira unachezwa na watu 11 kwa kila timu hivyo hao ambao wapo kwetu wapo tayari na imani yetu ni kwamba tutapata matokeo chanya.
“Tupo kwa ajili ya mchezo na matokeo yapo kwa timu ambayo itapambana. Ikumbukwe kwamba hii ni timu yetu wote na benchi la ufundi kazi yao ni kuona nani ataanza ili kupata ushindi,” amesema Canavaro.