VUGUVUGU kubwa kwa sasa ni kuelekea uchaguzi mkuu wa Shirkisho la Soka Tanzania, (TFF) ambao unatarajiwa kufanyika Agosti 7, huko Tannga.
Tangu kuanza kwa mchakato huo kumekuwa na purukushani za hapa na pale kwa kila mmoja kuvuta kasi kwake huku wimbo mkubwa ukiwa ni haki kwa kila mgombea kuzungumza mambo yake.
Ipo wazi kwamba wenye mamlaka ya kusimamia uchaguzi ni Kamati ya Uchaguzi ya TFF ambayo ina mamlaka ya kufanya masuala yote yanayohusu uchaguzi hivyo ni muhimu haki ikatendeka.
Ikumbukwe kwamba haki ikitendeka itafanya viongozi ambao watapatikana wawe na kazi kubwa ya kuleta maendeleo kwenye ulimwengu wa soka na hilo nina amini kwamba litakuwa sawa.
Rai yangu kwa wagombea pale ambapo wanaona kwamba haki haijatendeka basi wawasiliane na mamlaka husika ambazo zinasimamia uchaguzi kwani ikiwa itakuwa tofauti itakuwa na athari kwa Tanzania.
Ninapenda kuona kwamba mshindi ambaye atapatikana katika kila nafasi akawa amefuata utaratibu na yale magumu ambayo yameonekana kwa wakati huu yawe ni changamoto na yafanyiwe kazi.
Ukiachana na suala hilo bado ligi inaendelea kwa sasa kwa kila mmoja kusaka ushindi ndani ya uwanja hivyo muhimu kufanya maandalizi ili kupata ushindi.
Kwa wale ambao watashindwa kujipanga vizuri ni rahisi kukosa matokeo chanya na mwisho wa siku kuishia kwenye anguko lao jambo ambalo hakuna ambaye anapenda kuona ikitokea hivyo.
Upande wa waamuzi pamoja na wachezaji wote wanatakiwa kutenda haki ndani ya uwanja bila kujali wanacheza na timu gani kwani ni muhimu kwa wachezaji kujali haki na waamuzi kufanya maamuzi safi.
Hatupendi kuona kwamba matokeo yanapotoka kila timu inakuwa na malalamiko hiyo sio sawa tunahitaji kuona kwamba ligi inakuwa bora na yenye ushindani mkubwa kama ambavyo ipo kwa sasa.
Zipo ambazo kwa sasa zimeona mwanga wa kubaki kwenye ligi na nyingine zinaishi kwa hisia kwamba zipo kwenye ligi huku akili zao zikiwa Ligi Daraja la Kwanza.
Kilichobaki kwa sasa ni kumaliza hesabu zile ambazo zilikuwa zimepangwa kwa sababu hakuna ambaye anahitaji kuona timu yake ikipoteza mechi ambazo itacheza.
Ipo wazi kwamba zile ambazo zimeshindwa kufanya maandalizi mazuri ni lazima zitafeli na zitaangukia pua hilo lipo wazi hivyo ni muhimu kuwa na maandalizi mazuri kwa sasa.
Zimebaki mechi chache lakini hizi ni za muhimu kwa kuwa ukiachana na Mwadui FC ambayo ina uhakika wa kushiriki Ligi Daraja la Kwanza bado timu tatu zinatafutwa.
Jambo ambalo linahitajika kwa kila timu kwa sasa ni kuwa na nidhamu katika maandalizi na kupambana bila kuhofia katika kusaka pointi tatu.
Ukweli ni kwamba kwa sasa hakuna timu ambayo imekuwa nyepesi katika kutoa pointi tatu kwa kuwa tumeona kwamba hata timu ugenini zinashinda na nyingine zinafungwa zikiwa nyumbani.
Kinachotakiwa ni maandalizi kwa kila mchezo ili kuona namna gani ushindi utapatikana na hilo linawezekana kwa wachezaji pamoja na viongozi kuweka mipango sawa.
Pia ninapenda kuwapa pongezi wachezaji wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kwa kupata ushindi mbele ya Malawi kwenye mchezo wa kimataifa wa kirafiki uliochezwa Uwanja wa Mkapa.
Haikuwa kazi rahisi lakini wachezaji walijitoa na kupambana mwanzo mwisho hivyo inatakiwa kuwa hivyo siku zote pale mnapokuwa mmevaa jezi ya timu ya taifa ya Tanzania.
Kwa kufanya vizuri kwenye kwenye mechi ambazo mnacheza mnaongeza ile hamasa ya mashabiki kujitokeza kwa wingi pale ambapo mnacheza.
Mashabiki na benchi la ufundi wote mnastatahili pongezi kwa kuwa mmekuwa mkifanya vizuri hivyo mnastahili pongezi kwa kfanya kazi kwa umakini.