KOCHA mkuu wa kikosi cha klabu ya Simba, Didier Gomes amefunguka kuwa wamejipanga kucheza kama fainali mchezo wao ujao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga, ili kutangaza ubingwa wao wa nne mfululizo wa Ligi Kuu Bara.
Simba inayoongoza msimamo wa ligi na pointi zao 73 baada ya kucheza michezo 29, wanahitaji pointi tatu pekee kutangaza ubingwa wao wa nne mfululizo, huku wakijipanga kuwakaribisha Yanga katika mchezo wao ujao wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa Dar es Salaam Julai 3, mwaka huu.
Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wababe hao walipokutana, matokeo yalikuwa sare ya bao 1-1, mchezo uliopigwa Novemba 7, mwaka jana.
Akizungumza na Gomes amesema: “Tunafurahia kwa muendelezo wa ushindi tulionao, hii inazidi kutupa hali ya kujiamini kuelekea mchezo wetu ujayo dhidi ya Yanga.
“Tunatarajia kucheza mchezo huo kama fainali, ili kutangaza ubingwa wetu wa nne mfululizo, tuna michezo mitano mbele yetu na tunahitaji ushindi mmoja pekee, naiamini timu yangu na natumaini tutafanya vizuri mpaka mwisho wa msimu.
“Kuhusu Chama huyu ni mchezaji wetu muhimu, anakuwa na mchango mkubwa kikosini, tulipanga kumpa dakika 30 kwa ajili ya kuanza kumuandaa kuelekea michezo yetu ijayo, hasa ule wa nusu fainali dhidi ya Azam na pia mchezo dhidi ya Yanga.”