KWA kiasi fulani, taarifa za aliyekuwa Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji, kukosekana katika Mkutano Mkuu wa klabu hiyo uliopangwa kufanyika Jumapili hii, zinaweza kuwa mbaya kwa wapenzi na wanachama wa klabu hiyo.
Hatua hiyo inakuja baada ya Manji kurejea nchini hivi karibuni na kuleta matumaini kwa Wanayanga waliotarajia kumuona katika mkutano huo uliopangwa kufanyika Ukumbi DYCCC, Chang’ombe, Dar.
Yanga katika mkutano huo miongoni mwa ajenda zake zitakuwa ni mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo kwenda katika mfumo wa kisasa.Hivi karibuni, ziliibuka taarifa za Manji kulipia kadi ya uanachama ya klabu hiyo ambayo ingemruhusu kushiriki mkutano mkuu, lakini watu wake wa karibu, wamekanusha uwepo wa taarifa hizo.
Mtu wa karibu na Manji, amelithibitishia Spoti Xtra kwamba, kigogo huyo ataondoka nchini kabla ya kufanyika kwa mkutano huo, huku akiweka wazi kwamba, kiongozi huyo hakulipia kadi yake ya uanachama tangu atue nchini.
“Manji hakulipia ile kadi ya uanachama kama ambavyo watu wanasema, mwenyewe kabla ya mkutano mkuu kufanyika, atakuwa ameshaondoka hapa nchini, hivyo ni ngumu sana kwake kuwepo siku hiyo,” alisema mtu huyo.
Taarifa za Manji kukosekana katika mkutano huo, zitawashtua Wanayanga ambao wamekuwa na mapenzi makubwa na kiongozi wao huyo wa zamani ambaye hivi karibuni alirejea nchini baada ya kuondoka kwa muda mrefu kwani walipanga kumjadili kurudi kwake.
Manji aliwahi kuwa kiongozi wa Yanga kwa takribani miaka saba kuanzia 2012 hadi 2017 ambapo aliifanya timu hiyo kuwa tishio akifanikisha kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara tatu mfululizo kuanzia 2014 hadi 2016.