Home Simba SC SIMBA KUWAFUATA RUVU SHOOTING LEO

SIMBA KUWAFUATA RUVU SHOOTING LEO

 KIKOSI cha Simba kinachonolewa na Kocha Mkuu, Didier Gomes leo Juni Mosi kinatarajiwa kukwea pipa kuelekea Mwanza kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ruvu Shooting. 

Simba itawafuata Ruvu Shooting ikiwa na kumbukizi ya kunyooshwa bao 1-0 walipokutana Uwanja wa Uhuru.

Ilikuwa ni zama za Sven Vandenbroeck ambapo nahodha John Bocco katika mchezo huo alikosa penalti na kiungo wao mzee wa kukera Bernard Morrison alipigana na beki kisiki wa Ruvu Shooting,  Juma Nyosso.

Kutokana na kitendo hicho walipigwa faini ya laki tano pamoja na kufungiwa mechi tatu bila kucheza na Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF) kwa mujibu wa kanuni.

Mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na vita ya timu zote kupigania hesabu zao ambapo Ruvu Shooting wanahitaji kumaliza ndani ya tano bora na Simba inapigia hesabu ubingwa.

Kwenye msimamo Simba ina pointi 64 ikiwa nafasi ya kwanza inakutana na Ruvu Shooting yenye pointi 37 nafasi ya 10.

Unatarajiwa kuchezwa Juni 3, Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

SOMA NA HII  MGUNDA AWEKA MAMBO HADHARANI SAKATA LA ROBERTINHO NA PHIRI SIO POA, ISHU IKO HIVI