Home Yanga SC SIMBA vs YANGA | SHIKHALO KUSUSIWA GOLI LEO

SIMBA vs YANGA | SHIKHALO KUSUSIWA GOLI LEO


UHAKIKA ni kwamba Yanga itamuweka langoni kipa Faruk Shikhalo leo watakapokutana na Simba kwenye pambano la watani wa jadi, na kocha wake amefunguka kwamba angalau sasa anaanza kumuona kipa huyo wa miaka miwili nyuma enzi akitisha katika Ligi Kuu ya Kenya (KPL).

Akizungumza na gazeti la Mwanaspoti, Razack Siwa kocha anayenoa makipa wa Yanga na aliyewahi kufanya kazi na Shikhalo wakiwa Bandari ya Kenya na kipa huyo kuchaguliwa Kipa Bora wa Mwaka kwa misimu miwili mfululizo, alisema baada ya dakika 90 za nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC) dhidi ya Biashara United, Shikhalo ameonekana kuanza kuimarika na kujiamini langoni.

“Kikubwa ni kujiamini kuna wakati alikuwa ni kama kipa anayecheza akiwa na presha, hii inaweza kuwa labda kutokana na matokeo ya timu, ila kwa sasa yuko tofauti, naona anarejea katika kiwango ambacho nilikuwa nakijua anacho,” alisema Siwa na kuongeza;

“Kuna wakati nilikuwa simwelewi anajituma vyema katika mazoezi, lakini akija kwenye mechi anakuwa kama ana presha nikamuweka chini na sasa namuona anakuja kuwa Faruk yule niliyemtengeneza akiwa Kenya.”

Kocha huyo alisema anaamini Shikhalo atafanya vyema katika mechi ya Simba kwa kuwa hatakuwa mgeni kwenye mchezo kama huo na kwamba amewahi kutoka salama katika mechi kama hizo.

“Nimeangalia mkanda wa mechi yake ya kwanza ya msimu uliopita dhidi ya Simba ulioisha kwa sare ya 2-2 alicheza vizuri sana ile mechi, nikaangalia tena mechi ya kule Zanzibar nayo alifanya vizuri nimemwambia nataka kiwango bora zaidi ya kile alichoonyesha.”

Simba na Yanga leo zinakutana kwenye mechi yao ya 106 katika Ligi ya Bara tangu 1965, huku akiwa na nafasi kubwa ya kuanza akisubiriwa nje na Ramadhani Kabwili, kutokana na kipa namba moja Metacha Mnata kutumikia adhabu ya klabu yake na ile ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) iliyotokana na utovu wa nidhamu.

SOMA NA HII  YANGA SC YAIBUKA NA HILI...YAMFUA MORISSON SPESHO KWA AJILI YA SIMBA