NAHODHA msaidizi wa klabu ya Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ amesema upana wa kikosi chao ndio siri ya mafanikio makubwa waliyoyapata ndani ya misimu minne mfululizo.
Simba bora kila kona hilo linathibitishwa baada ya kutoa mfungaji bora wa ligi, John Bocco ambaye ameingia kambani mara 16, Clatous Chama ameibuka wimba aliyetoa pasi nyingi za mabao akihusika kwenye mabao 23 akitoa pasi na mwisho 15 na kufunga bao nane kati ya mabao 64 waliyofunga msimu huu.
Ukiachana na ubora wa washambuliaji Simba walikuwa imara pia kwenye safu ya ulinzi baada ya kuruhudu kufungwa michezo mitatu tu kati ya 34 waliyocheza.
Tshabalala amesema haikuwa rahisi kwao kupata mafanikio hayo juhudi, upambanaji ndio siri kuu huku akiweka wazi kuwa ubora wa mchezaji mmoja mmoja pia umekuwa chachu ya ubingwa mfululizo wa ligi na kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).
Amesema anaheshimu ubora wa kila mchezaji huku akiweka wazi kuwa Gadiel Michael ni bora anakaa nje kutokana na idadi ya wachezaji wanaotakiwa kuingia uwanjani.
“Wachezaji 11 ndio wanatakiwa kucheza hivyo kujituma mazoezini ndio siri ya kupangwa kikosi cha kwanza msimu huu kila mchezaji amecheza pamoja na kuonekana mimi bora,” amesema.
Akizungumzia ubingwa wa FA amesema wameupokea kwa furaha zaidi kutokana na kumfunga mtani wao na kutwaa taji mbele yao ni heshima kubwa kwao.