Home Makala SAWA KOMAA, LAKINI MANARA, BARBARA CHONDE

SAWA KOMAA, LAKINI MANARA, BARBARA CHONDE


Na Saleh Ally

UKIACHANA na suala la kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara mara nne mfululizo katika kipindi hiki, moja ya sifa kubwa kabisa ya Klabu ya Simba ni uongozi unaofuata weledi.

Simba ndio mfano wa uongozi kwa klabu nyingine, kwamba wanaendesha mambo yao kwa kufuata utaratibu sahihi kabisa kulingana na ubora wao.

Kweli kikosi chao ni bora, mambo yao yanaonekana yanakwenda kwa utaratibu mzuri kabisa katika kipimo sahihi na kila kitu ni kizuri.


Wengine wanapaswa kuanza kuiga au wameanza kuiga kutokana na wanavyosikia namna ambavyo Simba inaendeshwa. Kitu kizuri ni chachu ya mabadiliko na baadaye mafanikio kwa wengine.

Kwa sasa, mambo yanaanza kwenda tofauti na huenda ikaamka picha mpya kwamba inawezekana hata kwa watu wanaojitambua na kuendesha kazi zao kwa ufasaha kuanza kulumbana hadharani.


Kuna sauti ambayo imeanza kusambaa usiku wa kuamkia juzi, ikisikika Msemaji wa Simba, Haji Manara akimshutumu mambo kadhaa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez.

Maneno ni mengi na inaonekana katika shutuma hizo, Manara analia kudharauliwa, kunyanyaswa na kufanyiwa roho mbaya huku akisisitiza kwamba atazungumza baada ya mechi dhidi ya watani wao wa jadi Yanga kule Kigoma, Jumapili.

Manara ameendelea kueleza anavyokerwa na mambo kadhaa huku akitupa shutuma lukuki kwa Barbara ambaye ameendelea kuwa kimya.


Mchana kwenye ukurasa wake wa Instagram, ameeleza kwamba aliyevujisha sauti ile ni Barbara mwenyewe kwa kuwa yeye ndiye alimtumia. Akasisitiza aliamini anazungumza naye huku akiwa amejipanga kuzungumza baada ya mechi hiyo ya Kigoma, lakini sauti hiyo imevujishwa kwa makusudi.

Hilo ndiyo gumzo kubwa zaidi katika mchezo wa soka, wakati watu wanakwenda katika fainali ya Kombe la Shirikisho mjini Kigoma, sura imekuwa tofauti na sasa ni Manara wa Simba dhidi ya Barbara wa Simba. Jiulize!


Vipi iwe viongozi wa Simba walumbane katika kipindi kama hiki ambacho unatarajia kuiona timu hiyo ikijipanga vizuri kwa ajili ya kushinda mchezo huo?

Kati ya maneno aliyoyazungumza Manara ni kuhusiana na yeye kutuhumiwa kwenda kwenye kambi ya Yanga huku akisisitiza anadhalilishwa na bosi wake huyo ambaye amemuita ni anayependa umaarufu.

SOMA NA HII  ADAM SALAMBA: - NALIPWA MILIONI 161..AFUNGUKA JINSI ALIVYOJIUNGA NA TIMU YA MATAJIRI WA ALGERIA..ATAJA MADEM...

Yanga kwao wanaona ni kama hasira za mkizi au vita ya vifaranga vya kuku inayokwenda kuwa faida kwa kunguru au mwewe, jambo ambalo kwa Simba linawapitisha katika sifa mbovu kabisa.

Katika yale maneno, Manara mwisho alimaliza kwa kumueleza bosi wake huyo mwanamama “koma”. Lile neno linalomsisitiza mtu kuacha au kuachana na jambo fulani. 

Nami niwasisitize kwamba iwe hadharani au chinichini, bado wote hawakupaswa kuonyesheana nani zaidi kwa kipindi hiki.

Tunamuona Barbara akiwa amenyamaza, lakini kwa mujibu wa Manara alimshambulia kwa maneno kadhaa ambayo yanaonekana kumkera na kuanzisha mjadala huo ambao binafsi nauona hauna manufaa kwa Simba kwa kuwa wao wote wawili ni waajiriwa wa Simba hata kama ni kweli Barbara alisema yeye ndiye mwenye Simba kama alivyosema Manara. 

Kama viongozi ambacho walipaswa kukiangalia ni maslahi mapana ya kikosi cha Simba na Wanasimba wanaoizunguka klabu hiyo. Ikishinda ni faraja kubwa sana kwao na ikipoteza ni maumivu makubwa, sasa vipi waingize jambo linalopoteza mwendo wao unaopelekea umoja na mafanikio ambayo yamewapa sifa.

Sifa ya weledi inapotea, sifa ya uongozi bora kwao inapotea na hata lile jambo la kushindwa kwamba wanapaswa kulumbana wakati gani basi ni shida nyingine kubwa na litakuwa jambo bora wakikaa kimya, baadaye wakakutanishwa na ikiwezekana kuyaweka mambo sawa na waendelee.

Simba inaongozwa na watu ambao ndio wawakilishi wa kikosi chao. Dhamana waliyopewa ni kubwa sana, asiwepo anayeona ni zaidi ya mwingine, asiwepo atakayeona ni mkubwa kuliko klabu au bora sana zaidi ya wengine. 

Ikiendelea hivyo, watapoteza uelekeo na kuna siku, watashangaa kuona walipo ni chini ya wengine.

Kama kuna mgogoro, mazungumzo hayajawahi kushindwa na kama ni chuki za mioyo baina yao, basi kuna viongozi wanaoweza kufanya wakayamaliza lakini kwa kilichotokea, badala ya kuishia kwa Manara au Barbara kinaiangusha Simba yenyewe kuonekana imefeli kiuongozi.

Wote wawili mkome!